Home » » TAARIFA YA WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA TOKA WAJUMBE 201 KUHUSU MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA

TAARIFA YA WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA TOKA WAJUMBE 201 KUHUSU MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA

Written By peterdafi.blogspot.com on Wednesday, September 3, 2014 | 10:24 PM

Jana saa Sita Mchana hapa Dodoma, wajumbe wa Bunge la Katiba Kundi la
201 ambao wametoka katika makundi ya Kidini wamekutana na kutoa tamko
lifuatal;o kuhusu mwenendo wa Bunge la Katiba....

TAARIFA YA WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI WA BUNGE MAALUM LA
KATIBA TOKA WAJUMBE 201 KUHUSU MWENENDO WA SHUGHULI ZA
BUNGE MAALUM LA KATIBA

Sisi Wawakilishi wa Jumuiya na Taasisi za Dini, tuliopendekezwa na Taasisi
zetu na baadaye kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum
la Katiba, na kula kiapo cha utekelezaji wa jukumu hili kubwa.
Tukiamini kuandaa Katiba Mpya kwa maridhiano ya Kitaifa kwa wananchi
wote, tulipokea jukumu hili kama wajibu wetu Kitaifa. Aidha tunaamini
kwamba katika kupata maridhiano ya Kitaifa ni muhimu kuheshimu kila wazo
na fikra inayotolewa na kuunganisha fikra hizo kwa usahihi, kwa njia ya
kidemokrasia kwa kupiga kura na kukubaliana na matokeo ya wengi.
Kama ilivyoelezwa hapo awali, kabla ya kuanza shughuli za Bunge Maalum,
kila mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu na mtiifu kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na ufahamu wake,
kufanya kazi zinazomhusu, bila upendeleo na kumuomba Mwenyezi Mungu
amsaidie.

Tumeshangazwa na kusikitishwa sana kuona kwamba mchakato wa
kutayarisha Katiba itakayopendekezwa na Bunge hili kwa wananchi,
unachafuliwa taswira yake. Bunge Maalum la Katiba linachafuliwa na, shughuli
zake kuingiliwa na kupotoshwa na wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge,
Makundi, Taasisi na Vyombo mbali mbali vya habari, uhalali na ukweli wa
shughuli za BungeMaalum la Katiba unapotoshwa. Wananchi wanaaminishwa
yasiyo na ukweli.

Upotoshwaji huu umezua mijadala mbali mbali katika jamii ya Watanzania na
bado linaendelezwa kama ifuatavyo:

1. Kwamba Bunge Maalum la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe
wenzetu walioondoka wameliondolea uhalali wake kwa vile hwapo, wakiwepo
Bungeni basi uhalalai wake utakuwepo - utapatikana;
2. Inadaiwa kwamba Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo
ovyo;
3. Inadaiwa pia, kwamba kinachojadiliwa sasa katika Bunge hili ni Waraka
mwingine na si Rasimu iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
iliyowasilishwa rasmi Bungeni na kuanza kujadiliwa na wajumbe;
4. Inadaiwa na watu na Taasisi mbali mbali, kwamba viongozi wa dini,
wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, na wajumbe wa Kundi la 201,
wanapewa rushwa. Isitoshe Vyombo vya habari vimeandika tuhuma kama
hizi.
5. Inadaiwa pia kwamba wajumbe waliomo katika Bunge hili ni wachache,
ukilinganisha na hao walioko nje ya Bunge hilo;
6. Bunge hili, kwa tuhuma hizo, lazima lisitishwe au livunjwe na Mhe. Rais.
Kabla ya kuanza kuusahihisha upotoshwaji huo, sisi Wawakilishi wa Taasisi
za Dini mbali mbali na Wajumbe wa Kundi la 201 katika Bunge Maalum la
Katiba, tunapenda kufahamisha umma wa Tanzania mchakato wa kutayarisha
Katiba Mpya ulivyo kisheria.
Tunapenda kuwafahamisha Watanzania wenzetu kwamba mchakato huu una
hatua tatu kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mpaka hivi sasa ni
hatua moja imekamilika. Hatua ya pili ndiyo inayoendelea, na hatua ya tatu
bado haijaanza.

Hatua ya kwanza ni ile ya uandaaji wa Rasimu. Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura ya 83 iliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya kifungu cha
tano cha sheria hiyo. Tume hii ilipewa jukumu la kuratibu na kukusanya maoni
ya wananchi juu ya Katiba, kuanisha na kuchambua maoni ya wananchi na
kisha kuandaa rasimu ya Katiba. Kazi hiyo ilifanyika kwa kipindi cha takriban
miaka miwili na hatimaye Rasimu ya Katiba ilikamilika.
Hatua ya pili ilikuwa ni kuipeleka Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la
Katiba, ambalo liliundwa kwa shughuli maalum ya kuandika Katiba
inayopendekezwa, ili ifikishwe kwa wananchi ambao wataamua waikubali au
waikatae kwa kuwa wao ndio wenye maamuzi ya mwisho. Hawa ni
Watanzania wote wenye uwezo wa kupiga kura kwa kutoa maoni yao. Hoja ya
Mamlaka ya Bunge hili hatujazungumzia kwa vile imefikishwa Mahakama Kuu
ya Tanzania ili kupata tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hili. Tunachoweza
kusema ni kwamba jukumu kuu la Bunge hili ni kutengeneza Katiba
inayopendekezwa na Bunge ili ifikishwe kwa wananchi waipigie kura ya
maoni. Hatua hii ya pili bado inaendelea.
Hatua ya tatu ni pale Bunge Maalum la Katiba tutamkabidhi Mhe. Rais Katiba
inayopendekezwa ambayo itafikishwa kwa wananchi ili waikubali kama
wataridhika nayo au kuikataa kama haikidhi matarajio yao.
Hatua hii ni ya mwisho wananchi wakiikubali tunapata Katiba Mpya
wakiikataa, tunaendelea na Katiba tuliyonayo.
Kilichotokea ni kwamba, wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge hili wameamua
kuukiuka utaratibu uliowekwa kisheria. Badala yake wamepeleka Rasimu ya
Katiba kwa wananchi wakati mchakato wa kutayarisha Katiba
inayopendekezwa bado haujakamilika.
Sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na
kuusimamia ukweli ni moja ya majukumu yetu katika jamii, tumesikitishwa
sana na taarifa potofu zinazosambazwa kwa makusudi na makundi, taasisi na
vyombo vya habari mbali mbali na tukiwa wajumbe wa Bunge hili ambao
tunafahamu kwa kina na tunaridhika na kila hatua ya mchakato huu. Tuna
wajibu wa kusahihisha upotofu huu, unaoendeshwa kwa makusudi na hivi
kuwaeleza Watanzania ukweli na hali halisi inayojiri hapa Bungeni.
Watanzania msifadhaishwe na wala msibabaishwe. Hali ni shwari. Mchakato
unaendelea kwa amani na utulivu.
Katika kusahihisha upotofu unaozungumzwa kupitia mijadala na midahalo
mbali mbali katika jamii, tunaomba kufafanua hali ilivyo kama ifuatavyo:-

TUHUMA KWAMBA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUKOSA UHALALI
Jambo hili si kweli hata kidogo kwani kuna wajumbe wa aina tatu Bungeni
ambao wamewekwa na kutambuliwa kisheria. Hawa ni kama wafuatao:
1. Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
3. Wajumbe 201 walioteuliwa na Mhe. Rais, baada ya kupendekezwa na
Taasisi, Mashirika na makundi mbali mbali nchini,
Uhalali wa Bunge unakuwapo wakati wajumbe kutoka makundi hayo matatu
wapo Bungeni, na si Vyama vya Siasa pekee. Iwapo kwa mfano wajumbe wa
201 wakiamua kutoshiriki katika shughuli za Bunge, basi sehemu moja
muhimu ya Bunge haitakuwapo na uhalali wa Bunge hautakuwepo.
Hata hivyo, Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zimeweka idadi ya akidi
ambayo ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalum. Akidi hii ikifikiwa Bunge
huendelea na shughuli zake. Akidi hii hufikiwa kila wakati BungeMaalum
linapokutana. Hii inamaanisha kwamba Bunge Maalum la Katiba linaendesha
shughuli zake kwa misingi ya sheria na taratibu zilizojiwekea. Bunge lina
uhalali wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.

TUHUMA KWAMBA KANUNI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA ZINAVUNJWA
Suala hilo halijawahi kutokea. Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zilipitishwa
na wajumbe wote kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sheria
Namba 83. Vile vile uendeshaji wote wa shughuli za Bunge zinafanywa kwa
mujibu wa Kanuni za Bunge Maalum. Kanuni hizo zinatoa fursa ya Bunge
Maalum kuzirekebisha pindi inapobainika ipo haja ya kufanya hivyo kwa
mujibu wa kanuni Namba 87.

WARAKA MWINGINE UNAJADILIWA NA SI RASIMU YA TUME
Hili nalo si kweli. Tunawahakikishia Watanzania wote kwamba sisi kama
Wawakilishi wa Taasisi za Dini miongoni mwa wajumbe wa Kundi la 201, kwa
ujumla tunasema hii si kweli. Ni upotoshaji wa makusudi. Tunaijadili Rasimu
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ibara kwa ibara. Ibara nyingi zimeachwa
kama zilivyo. Kuna ibara ambazo zimeboreshwa au kurekebishwa, kuna
ambazo zimeondolewa na kuna nyingine mpya ambazo zimewekwa ili kuweka
mambo ya msingi ambayo Rasimu haikuyazingatia au haikuyaona.

WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI, WAJUMBE WA KUNDI LA 201 WA BUNGE
LA KATIBA KUPEWA AU KUPOKEA RUSHWA
Sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini na Wajumbe wa Kundi la 201 wa Bunge
hili tumesikitishwa sana na taarifa hii iliyosambazwa na baadhi ya watu, na
kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari aidha kupitia kwenye mijadala,
midahalo na makongamano mbali mbali. Baadhi yetu sisi Viongozi wa Kiroho
tumeapishwa viapo vya uadilifu katika uongozi wetu wa kiroho na tuko mstari
wa mbele kuongoza waumini wetu kuepuka dhambi ya tamaa ya fedha, na
kusema uongo. Taarifa kama hizo hazionyeshi heshima kwa dini au nafasi
zetu za kipekee katika uongozi wa kiroho. Taarifa hizi zinatangazwa kwa
makusudi na watu mbali mbali kupita vyombo vya habari kwa malengo ya
kisiasa na kutudhalilisha sisi Viongozi wa kiroho mbele ya umma. Tunaomba
tabia hii ikomeshwe.

TUHUMA KWAMBA BUNGE KUWA NA WAJUMBE WACHACHE
Hili nalo si kweli. Wajumbe wanaohudhuria Bunge wanakidhi akidi
inayohitajika kwa mujibu wa kanuni.

HOJA YA KUSITISHWA AU KUVUNJWA KWA BUNGE MAALUM
Hii ni hoja inayozungumzwa katika mijadala mbali mbali katika jamii. Msingi
wa hoja hiyo ni kutokuueleza umma ukweli ulioko Bungeni kwa kupeleka
taarifa potofu kwa wananchi kwamba Bunge Maalum limekosa mwelekeo.
Hatuoni sababu za hoja hii kutiliwa maanani kwa kuwa hakuna sababu za
msingi na za kisheria za kufanya hivyo.

HITIMISHO
Kumekuwa na taarifa mbali mbali zenye malengo ya ama kuingilia shughuli za
Bunge hili au kutudhalilisha sisi wajumbe ambao si Wabunge au Wawakilishi.
Wajumbe 201, ambao mchango wao katika mijadala ya Kamati mbali mbali
umekuwa na uzito wa pekee, hautambuliki katika taarifa hizo ambazo zimejaa
malengo ya kisiasa zaidi kuliko ukamilishaji wa shughuli za Bunge Maalum.
Kuna taarifa nyingine zimesambazwa zikiwa na upotoshaji mkubwa, licha ya
kwamba Taasisi zinazosambaza taarifa hizo zina wajumbe wake katika Bunge
Maalum. Wajumbe hao wangeweza kuzielimisha Taasisi zao ukweli ulipo hapa
Bungeni, na hivyo kuwafikishia wasomaji wao taarifa zilizo za kweli na ili
kulijengea Bunge hili heshima machoni pa umma wa Tanzania na Kimataifa.
Udhalilishaji kama huu unatuumiza hata sisi wajumbe ambao kwa hiari yetu
tuliamua kubaki Bungeni na kuyatimiza hayo ambayo tulitumwa tuje
tuyakamilishe.

Kama tulivyosema hapo awali ni wajibu wetu kama Viongozi wa Dini na
Wajumbe wa Bunge hili kuutaarifu umma hali halisi katika shughuli za Bunge
Maalum na kuwasihi wapotoshaji kwamba wauheshimu ukweli na
wawaheshimu watanzania kwa kuwaeleza ukweli.
Ahsanteni sana.
……………………. …………………………
SHEIKH HAMID MASOUD JONGO ASKOFU AMOS JOSEPH MUHAGACHI
BAKWATA KIKRISTO
TAREHE 3 SEPTEMBA, 2014

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger