MAELEZO YA MHE. UMMY A. MWALIMU (MB.) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI ULIFANYIKA KATIKA UKUMBI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU KUHAMASISHA WAZAZI /WALEZI JUU YA WATOTO KUJIUNGA NA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI KWA MWAKA 2016
Ndugu wanahabari;
Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia uzima na kuweza kukutana hapa katika wiki ya kwanza ya mwaka 2016. Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa kuhudhuria mkutano huu ambao kupitia kwenu nitapata fursa ya kuhimiza wazazi na walezi juu ya ”Watoto kujiunga na Elimu ya Msingi na Sekondari”.
Ndugu Wanahabari,
Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 asilimia 51 ya watanzania ni Watoto, hivyo kundi hili ni nguzo kuu ya Taifa na njia ya kumjengea mtoto msingi imara wa maisha yake ni kumpatia elimu. Kuwekeza kwenye elimu ya mtoto kuna mchango mkubwa katika kukuza upeo wa akili, uelewa, ufahamu, ubunifu na udadisi wa mazingira kadri umri unavyoongezeka.
Katika umri huu mdogo watoto hurithishwa maadili mema na maarifa ili kuwa na Taifa lenye raia wema walioandaliwa kudumisha uzalendo, amani, uadilifu, uaminifu, kujiamini, na kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa. Hivyo mtoto anahaki ya kuendelezwa kwa kupatiwa elimu bora kwa ajili ya kujenga msingi imara wa maisha yake, familia na jamii kwa ujumla.
Ndugu Wanahabari,
Serikali inaamini kuwa ikiwa tunataka kujenga Taifa lililoelimika ni lazima kuwekeza kwenye elimu. Kwa kutambua hilo, mnamo mwaka 1990 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto uliosainiwa mwaka 1991, pamoja na Itifaki zake za nyongeza. Mkataba huo pamoja na mambo mengine, unasisitiza utoaji wa elimu ya msingi bure kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote ile.
Vilevile, Serikali imekuwa ikitekeleza Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 inayosisitiza utoaji wa Haki za Msingi za Mtoto ikiwemo haki ya kupata elimu. Aidha, katika kuonesha utashi wa dhati wa kuendeleza haki ya elimu kwa watoto; Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John P. Magufuli wakati wa Kampeni aliahidi kuwa atahakikisha elimu ya msingi na ya Sekondari itatolewa bure kwa watoto wote nchini. Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa napenda kumpongeza na kumshukuru Mhe Rais kwa kutekeleza ahadi yake kwa haraka. Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo tayari pesa zimeshatumwa kwa kila shule kwa ajili ya utekelezaji. Sasa ni muhimu kila mmoja wetu na wadau wengine kuhakikisha watoto wananufaika na fursa / nia hii njema ya Mhe Rais ya kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bure.
Ndugu Wanahabari,
Tufahamu kuwa Mwezi huu wa Januari 2016 Muhula wa masomo kwa Shule za Msingi na Sekondari (O-level) unaanza. Kwa Mujibu wa Taarifa kutoka TAMISEMI tunatarajia Watoto zaidi ya Milioni moja wataandikishwa kuanza masomo ya elimu ya shule za Msingi mwaka huu wa 2016 na watoto takriban laki tano watajiunga na sekondari. Hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kutumia fursa hii kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume wanapata elimu ya msingi na sekondari. Ninalisema hili kwa sababu Wizara yangu ina wajibu wa Kuhakikisha Watoto wanapata Haki zao za Msingi ikiwemo haki ya kupata Elimu.
Ndugu Wanahabari,
Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi ,Teknologia na Ufundi itaendelea kuhamasisha Wazazi / Walezi kutimiza Wajibu wao wa kuhakikisha kuwa Watoto wote wenye umri wa kuanza shule za Msingi na Sekondari wanaanza kwa wakati.
Vile vile, Wizara yangu itaweka Msititizo kwa Wazazi / Walezi wenye watoto wa umri kati ya miaka mitatu hadi mitano kutimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto hao kwa ajili ya kujiunga na elimu ya awali.
Ndugu Wanahabari,
Katika kuhakikisha kwamba kuna mwitikio mkubwa wa watoto wanaoanza masomo ya darasa la kwanza na Kidato cha kwanza mwaka huu 2016, ninasisitiza yafuatayo:-
Wazazi/ Walezi / Jamii kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kuanza Elimu ya Msingi yaani Darasa la Kwanza na elimu ya awali wanajiunga na shule kwa muda uliopangwa na kuhudhuria masomo ipasavyo. Na Endapo Mzazi/ Mlezi hajaandikisha Mtoto mpaka sasa muda bado upo, ni vyema afanye hivyo haraka. Wajibu huu upo vile vile kwa wazazi / walezi wenye watoto wanapaswa kujiunga na Kidato cha Kwanza.
Wazazi, Walezi na familia zenye Watoto wenye mahitaji maalum kuhakikisha watoto wanapelekwa shule ili kutoa haki sawa ya elimu kwa watoto wote.
Wananchi wote washirikiane na watendaji wa Serikali katika kuunga mkono zoezi hili. Ninawaomba wananchi kufichua taarifa za watoto wote wenye umri wa kwenda shule, ambao hawakuandikishwa na ambao hawatahudhuria masomo.
Aidha, ninaagiza yafuatayo kwa Viongozi na watendaji:-
Viongozi na Watendaji wa Mikoa na Halmashauri wawasimamie Maafisa Maendeleo ya Jamii na watendaji wa kata kutekeleza majukumu yao ya kuhamasisha jamii ipasavyo juu ya watoto kujiunga na darasa la kwanza na kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa 2016.
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa, Halmashauri na Kata ninahitaji msimamie utekelezaji wa Agizo hili. Hakikisheni kuwa Agenda yenu kubwa katika kazi zenu kwa Mwezi wa Januari na februari iwe ni kuhamasisha wazazi na walezi kuwapeleka shule watoto wenye sifa za kujiunga na elimu ya msingi na Sekondari. Ninahitaji nipate taarifa ya utekelezaji wa jambo hili mwishoni mwa mwezi Februari 2016.
Hitimisho:
Elimu ndio njia bora ya kuwajengea watoto wetu msingi imara wa maisha yao. Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wazazi/walezi ambao watazembea, kumficha, kumtorosha au kuzuia mtoto kuanza masomo ya shule za msingi na sekondari.
Aidha, natoa rai kwa wazazi na walezi wote kuhakikisha kuwa watoto wote wanaoendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari wahudhurie masomo yao kwa ufanisi. Serikali haitarajii kuendelea kuona utoro wa watoto mashuleni kutokana na sababu zinazoweza kuepukika.
Napenda ifahamike kuwa Ifikapo tarehe 30 Machi 2016, Serikali kupitia Ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali itawafungulia Mashitaka na kuwapeleka Mahakamani Wazazi na Walezi wote watakao shindwa kutimiza wajibu wao wa kupeleka watoto wao shuleni ili kupata Elimu ya Msingi na Sekondari.
Sheria ya Mtoto Namba 2 ya mwaka 2009 Kifungu cha 8, inaelekeza kuwa Ni wajibu wa mzazi kuhakikisha Mtoto anapata elimu.
Kifungu cha 14 kinatamka kuwa ni Kosa la jinai kushindwa kutimiza wajibu huo. Adhabu yake ni faini isiyozidi milioni 5 na kifungo kisichozidi miezi 6 au vyote.
Hivyo, Wazazi/Walezi tutimize wajibu wetu kwa maendeleo ya watoto wetu na Taifa letu kwa ujumla.
‘KWA PAMOJA TUWAPE WATOTO HAKI SAWA YA ELIMU’.
.... AHSANTENI SANA ....
Post a Comment