NAIBU Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto amesema asilimia 15 ya wanawake wamegundulika kuwa wamekeketwa na kwamba takwimu hizo zinaonyesha pia kuwa ukeketaji huo umekithiri katika mikoa minane hapa nchini.
Naibu Waziri huyo,Dk.Hamisi Kigwangala ametoa takwimu hizo alipokuwa akifunga kongamano la siku ya kupinga vitendo vya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wanawake lililofanyika mjini hapa.
Alifafanua naibu waziri huyo kuwa takwimu hizo zinaonyesha kwamba ukeketaji huo umekithiri katika mikoa ya Manyara,Dodoma,Arusha,Singida pamoja na mkoa wa Mara na kwamba ukubwa wa tatizo hilo katika mikoa hiyo linatokana na imani na mila potofu.
“Kwa mujibu wa utafiti wa kidemografia na Afya Tanzania (Tanzania Demographic and Health Survey) wa mwaka 2010 unaonyesha kuwa asilimia 15 ya wanawake wamekeketwa na kwamba takwimu hizo zinaonyesha ukeketaji umekithiri katika mikoa ya Manyara asilimia 71”alisema.
Aliitaja mikoa na asilimia zake kuwa ni mkoa wa Dodoma asilimia 64,Arusha asilimia 59,Singida asilimia 51 na Mara asilimia 40 huku akiweka bayana kuwa takwimu hizo zinaonyesha pia ukubwa wa tatizzo la ukeketaji katika mikoa ya Dar-es-Salaam,Morogoro na Pwani kutokana na watu wa makabila mbali mbali kuhamia katika mikoa hiyo.
“Serikali inapinga,kulaani na kukemea tabia ya kuendelezwa kwa vitendo hivi vya ukatili unaomdhalilisha mtoto wa kike kwani unamsababishia madhara makubwa kiafya,kielimu, kisaikolojia na kimaendeleo”alisisitiza Dk.Kigwangala.
Post a Comment