Home » » MAELEZO YA MHE. UMMY ALLY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA KATIKA HAFLA YA KUPOKEA MSAADA WA FEDHA KWA AJILI YA KUWEZESHA MATIBABU YA WAGONJWA WA MOYO KATIKA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

MAELEZO YA MHE. UMMY ALLY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA KATIKA HAFLA YA KUPOKEA MSAADA WA FEDHA KWA AJILI YA KUWEZESHA MATIBABU YA WAGONJWA WA MOYO KATIKA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

Written By peterdafi.blogspot.com on Wednesday, March 2, 2016 | 1:20 AM

MAELEZO YA MHE. UMMY ALLY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA HAFLA YA KUPOKEA MSAADA WA FEDHA KWA AJILI YA KUWEZESHA MATIBABU YA WAGONJWA WA MOYO KATIKA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE TAREHE 2/3/2016

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Kaimu Mkurugenzi, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete  (JKCI),
Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Wakuu wa Idara - Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete  (JKCI),
Watumishi wote mliopo,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujali afya njema na hatimaye ametuwezesha tukusanyike mahali hapa. Vile vile, nitumie fursa hii kuwashukuru watumishi wote wa Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya ya utoaji wa huduma za afya kwa watanzania wote. Pia, nitumie nafasi hii kuwapongeza ndugu zetu wa Jumuiya ya Kihindu ya hapa Dar es Salaam ijulikanayo kama BAPS, kwa kuguswa kwao na kutoa msaada mkubwa na upendo waliouonyesha kwa watanzania hawa wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo.

Ndugu Wanahabari,
Nimeafiriwa kuwa kiasi cha msaada unaotolewa utawezesha wagonjwa wapato 100 kupatiwa matibabu ya moyo. Hii ni faraja kubwa kwa wagonjwa wetu waliokuwa wakisubiri huduma hizi kwa muda mrefu.

Ndugu Wanahabari,
Takwimu zinaonyesha kuwa, kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo, kisukari, n.k. Wizara yangu imejipanga kuhakikisha kuwa inaweka mkazo katika kutoa elimu ya kujikinga na maradhi mbalimbali ili kuokoa maisha ya watanzania walio wengi. Ni dhahiri kuwa gharama za matibabu zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku. Hivyo, nitoe rai kwa watanzania wote, tujaribu kuzingatia Kanuni za Afya kama kufanya mazoezi, kula vyakula kwa kuzingatia mahitaji ya miili yetu, na kupima afya zetu mara kwa mara.

Ndugu Wanahabari,
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikiendesha huduma hizi za kambi, kila inapoona kuna ongezeko la wagonjwa wanaohitaji tiba za aina hii.  Kitendo hiki ni kizuri kwa kuwa kinawezesha wananchi/wagonjwa kupata huduma hii kwa haraka zaidi. Ni matarajio yangu kuwa kambi itakayoanza tarehe 7/3/2016, itanufaisha wagonjwa wengi zaidi ikiwezekana nusu ya wagonjwa hao wanaosubiri huduma hii.

Ndugu Wanahabari,
Mmetaarifiwa kuwa wagonjwa waliopo sasa wanatoka karibu kila pembe ya nchi yetu, mathalani katika wagonjwa watakaofanyiwa matibabu, wagonjwa 10 wanatoka Zanzibar na waliobaki wanatoka Tanzania Bara.

Lengo la Serikali ni kuboresha huduma za Tiba za Rufaa nchini ili kupunguza idadi ya rufaa za wagonjwa nje ya nchi. Mfano: kati ya mwaka 2000 hadi 2014 jumla ya wagonjwa 7,363 walipewa rufaa kwenda kutibiwa nje ya nchi sawa na wastani wa wagonjwa 526 kwa mwaka ambapo kati yao wagonjwa 4,413 sawa na wastani wa wagonjwa 315 kwa mwaka waliweza kwenda nje ya nchi kwa matibabu. Aidha, kati ya mwaka 2012 na 2015 wagonjwa 1465 walitibwa nje ya nchi kwa gharama za Serikali. Karibu asilimia 50 ya wagonjwa waliotibiwa nje ya nchi kwa gharama za Serikali kati ya mwaka 2012 hadi Novemba, 2015 walikuwa wanaugua magonjwa ya moyo. Kutokana na ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo Serikali mwaka 2008 iliamua kuanzisha huduma za upasuaji mkubwa wa moyo na hatimaye kujenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambayo ilianza Aprili, 2015. Tangu kuanza kwa Taasisi hii, kambi maalumu za upasuaji moyo zimekuwa zikiendeshwa na wataalamu wa hapa nchini kwa kushirikiana na wa kutoka nje ya nchi ambapo jumla ya wagonjwa 247 wamefanyiwa upasuaji wa moyo. Kambi za upasuaji zimesaidia kupunguza idadi ya wagonjwa ambao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu. Aidha, hatua hii imepunguza gharama kwa Serikali kwa sababu idadi ya wagonjwa wa moyo waliopata rufaa imepungua toka 198 hadi 89 kati ya mwaka 2013 na Novemba 2015.

Matibabu nje ya nchi yana gharama kubwa ambazo zinatofautiana kulingana na ugonjwa husika. Gharama za kumtibu mgonjwa mmoja wa moyo ni Shs.16,500,000.00 mgonjwa mmoja wa figo ni Shs.57,750,000.00 na mgonjwa mmoja wa saratani ni Shs.74,250,000.00. Matumizi ya fedha kwa ajili ya matibabu nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka kulingana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa. Kuongezeka idadi ya wagonjwa wa rufaa kumesababisha Serikali kuwa na limbikizo la deni lililofikia Shs.28,743,586,356/= hadi kufikia mwezi Desemba, 2015.

Hitimisho:
Kabla sijamaliza maelezo yangu, nitoe shukurani za dhati kwa Madaktari na Wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete  (JKCI). Kipekee kabisa niwashukuru Jumuiya ya Kihindu ya BAPS kwa msaada mkubwa walioutoa katika kuhakikisha wanaokoa maisha ya watanzania hao, niendelee kuwaomba pale mtakapoguswa zaidi, saidieni katika maeneo mengine pia kama ununuzi wa vifaa tiba na ikiwezekana basi msaidie ili wagonjwa waliobaki wapate tiba wote hapa nchini. Huu ni uzalendo wa hali ya juu na tunashukuru kwa kumuunga mkono Mhe. John Pombe Magufuli Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma zote za msingi kadri inavyowezekana siku zote tunasema “kutoa ni moyo usambe si utajiri”.

Asanteni kwa kunisikiliza. 

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger