Kama ilivyokuwa kwa binadamu wengine, wakazi wa eneo ambalo hatimae limekuwa nchi yetu ya Tanzania, walikuwa na utamaduni wao. Utamaduni huu ulikuwa ukitofautiana kati ya kabila na kabila. Moja ya vipengele ilikuwa muziki. Kabla sijaendelea ni habari hii ni vizuri tukumbuke jambo moja, ikiwa kitu hakiko katika utamaduni wa kundi la watu, kitu hicho huwa hakina jina katika kundi lile. Nikiuliza unambie internet kwa kabila lako inaitwaje hutakuwa na jina hilo kwa kuwa hakuna kitu hicho katika utamaduni wa kabila lako. Hatukuwa na ‘muziki’ katika makabila yetu kabla ya ujio wa wageni, na hivyo hakuna kabila lenye tafsiri ya neno muziki. Lakini tuliimba, tulicheza ngoma, tulipiga vyombo mbalimbali, ila tulikuwa na utamaduni mwingine kuhusu kitu hiki tunachokiita siku hizi muziki. Watafiti wanatuambia tulikuwa na Ngoma, ambayo tafsiri yake ni kubwa kuliko muziki. Ngoma ilikuwa ni chombo kile kilichotoa muziki, ngoma ilikuwa shughuli yenyewe, kwa mfano ngoma ya mavuno, ngoma ya mashetani na kadhalika, na pia tulicheza ngoma. Sina taarifa ya maandiko yenye kina kuhusu hali ya ngoma katika kipindi hicho lakini tunajua watu waliimba na kucheza ngoma kwa matukio mbalimbali, hali ambayo inaendelea mpaka leo.
WAKATI WA MKOLONI
MJERUMANI
Wajerumani ndio waliotuletea neno muziki, na katika wakati wao ndipo kuliingia muziki wa bendi za askari na kuingizwa katika shule ya kwanza ya serikali wakati huo, Tanga School. Katika kipindi hiki pia mchango wa madhehebu mbalimbali kuingiza muziki na vyombo vya muziki vipya ulitoa mchango katika kuongeza kasi ya huu muziki mpya. Pengine unaweza ikasema kuwa kipindi hiki kwaya nazo zilianza kushika kasi, hapa kama nilivyosema mwanzo neno kwaya pia ni jipya lililotokana na neno la Kiingereza choir. Historia intueleza kuwa Mjerumani hakufanya jitihada za kuzuia muziki wa kiasili, hivyo basi muziki mpya na wa kiasili ulienda sambamba
MUINGEREZA

BAADA YA UHURU MIAKA YA 60/70
Pamoja na mapungufu yanayotajwa ya utawala wa chama kimoja, kulikuweko na mambo yaliyowezekana kutokana na hali ya chama kimoja kuwa na dira inayoeleweka na hivyo kuelekeza kila kitu kadri ya matakwa ya chama. Sanaa ya Tanzania haikukwepa mwongozo wa TANU, sehemu za kazi , vijiji , miji viliagizwa kuwa na vikundi vya ‘utamaduni’ ambavyo vingekuwa ndio vikundi vya burudani baada ya kazi na pia jukwaa la kuelezea mipango na malengo ya chama na serikali. Zikatengenezwa bendi za majeshi, polisi, JWTZ, Magereza, Uhamiaji, mashirika ya umma nayo hayakuwa nyuma, BIMA, TANCUT, DDC Mlimani, UDA na miji nayo ikawa na bendi Kurugenzi Arusha Kurugenzi Dodoma. Na ni ukweli usiopingika nyimbo nyingi maarufu kama zilipendwa zilipatikana katika kipindi hiki.
Bendi zilitunga nyimbo, ambazo zilipitia katika kamati iliyozipitia kabla ya kuruhusiwa kurekodiwa na kurushwa hewani. Kwa upande wake serikali nayo ikatengeza idhaa tatu katika redi ya taifa, External Service, iliyokuwa ikitangaza kwa lugha ya Kiingereza na lugha ya nchi za kusini zilizokuwa zikipigania uhuru wakati huo, kukaweko na Idhaa ya Biashara ambayo ilikuwa na vipindi vikitangaza biashara mbalimbali vilivyodhaminiwa na wafanya biashara, katika idhaa hii, uliweza kusikia muziki kutoka popote duniani, lakini kwa makusudi kabisa kukaweko na idhaa ya Taifa ambako huku ungesikia kila aina ya muziki wanchi hii, pamoja na kuwa kwa sasa kuna vituo vya radio zaidi ya 80 vimeshindwa kufanya kazi hii iliyoweza kufanywa na kituo kimoja cha Taifa, bahati mbaya kituo hicho cha Taifa kimeshapoteza muelekeo wake huu uliokuweko awali.
Katika miaka ya mwanzoni ya 60, bendi ziliingia katika utamaduni wa kunakili nyimbo kutoka Kongo, kilichofanyika ni kuimba Kiswahili tu, kuna nyimbo kama Napenda nipate lau nafasi, Mtoto wacha kupiga mayowe na nyingi sana ambazo zilikuwa ni za kunakili moja kwa moja nyimbo za Kongo. Hali ilifikia kuwa mbaya mpaka bendi nyingine ziliingilia kati na kutunga nyimbo za kuwaasa wenzao watunge nyimbo zao....Koma koma koma kaka wewe tunga zako.. ilikuwa baadhi ya maneno ya kuwafanya wanamuziki waliokuwa wakiiga waache kuiga. Lakini pamoja na haya kulikuweko na wanamuziki waliokuwa wakiangalia na kuiga nyayo kutoka nchi za magharibi na baadae wakichanganya vyombo na melody za kiasili na kuanza muziki uliojulikana kama Afro Rock, na kuwa sambamba na nchi nyingine katika Afrika. Katika kipindi hiki mwanasiasa mmoja aliwahi kupiga marufuku muziki wa bugi, ambao ulikuwa ni maonyesho ya muziki ya mchana yaliyokuwa yakisha saa kumi na mbili, na kwa kupiga marufuku muziki huo ilikuwa ni sawa leo upige marufuku wanamuziki wa kizazi kipya, pengo aliloliweka halijaweza kujazwa tena.
MIAKA YA 80/90
Katika kipindi hiki kulikuweko na mfumo wa utawala wa shughuli za Utamaduni ambao pamoja na kuweko Maafisa Utamaduni wa Wilaya, Maafisa Utamaduni wa Mkoa , pia kulikuweko na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), ambapo kulizaliwa vyama ambavyo vilifanya kazi kubwa katika kuunganisha wanamuziki kama vile CHAMUDATA na Tanzania Taarab Association. Na itakuwa ni makosa kutotaja show iliyokuwa kubwa sana na iliyounganisha wanamuziki wa nchi nzima TOP TEN Show. Show hii iliyowezekana kwa ushirikiano wa BASATA, Umoja wa Vijana, Radio Tanzania, halijawahi kutokea tena onyesho lenye ukubwa wa aina hiyo mpaka leo. Kuvurugika kwa mfumo wa uongozi wa utamaduni kwa kuwaondoa Maafisa Utamaduni walioko chini ya Wizara ya Utamaduni umeacha shughuli za Utamaduni mkononi mwa wafanyabiashara pekee, ambao kwao lengo ni kupata faida za kiuchumi, matatizo na mtokeo ya kufa kwa utamaduni si lolote kwao.
Serikali inatakiwa ichukue mzigo huu wa kufadhili ukuaji na uendelezaji wa Utamaduni, na kuacha shughuli za biashara ya kazi za sanaa kwa wafanya biashara.
Post a Comment