Dk. Slaa
HATIMA ya ndoa ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa na mpenzi wake, Josephine Mushumbusi sasa itajulikana leo.Mahakama Kuu leo inatarajia kutoa uamuzi juu ya pingamizi la awali lililotolewa na Dk Slaa akisema mlalamikaji, Rose Kamili hana haki ya kupinga asifunge ndoa.
Dk Slaa na Josephine walitarajia kufunga ndoa kwenye Kanisa Katoliki Julai 21, mwaka huu, lakini Rose anayedai kuwa alikuwa mkewe, alifungua kesi hiyo kupinga ndoa hiyo na kudai fidia ya Sh550 milioni.
Hata hivyo, Dk Slaa pia kupitia kwa wakili wake, Phillemon Mutakyamirwa aliweka pingamizi la awali (PO), dhidi ya Rose akidai kuwa hana haki ya kufungua kesi kupinga yeye kufunga ndoa na Josephine, huku akiomba mahakama ifutilie mbali kesi hiyo.
Jaji Laurence Kaduri anayesikiliza kesi hiyo, atatoa uamuzi wa pingamizi hilo la awali la Dk Slaa, baada ya kusikiliza hoja katika pingamizi hilo pamoja na hoja za utetezi dhidi kupitia majibu ya Rose, zilizowasilishwa mahakamani hapo kwa njia ya maandishi.
Umuzi huo ndio utakaotoa hatima ya ndoa hiyo, kwani iwapo mahakama hiyo itakubaliana na pingamizi hilo la awali la Dk Slaa, basi kesi hiyo itatupilia iliyofunguliwa mahakamani na Rose itatupwa na badala yake Katibu huyo Mkuu wa Chadema atakuwa huru kufunga ndoa.
Ikiwa mahakama itatupilia mbali pingamizi hilo la awali la Dk Slaa, basi ndoa hiyo itakuwa mashakani kufungwa kwa kuwa iatasubiri uamuzi wa kesi iliyofunguliwa na Rose.
Katika pingamizi hilo, Dk Slaa anadai kuwa hawakuwa na ndoa halali kisheria na Rose na kwamba ndoa hiyo ni dhana tu ambayo haiwezi kumfanya awe na nguvu ya kumpinga kufunga pingu za maisha na Josephine.
Akitoa ufafanuzi wa pingamizi hilo, Wakili wa Dk Slaa Phillemon Mutakyamirwa alisema kuwa kutokana na sababu hiyo, Rose hakupaswa kufungua kesi mahakani kupinga Dk Slaa kufunga pingu za maisha na Josephine kisheria
Post a Comment