Nilikuwa
katikati ya kazi jimboni nikaambiwa kwamba kuna mwito humu wa Nape na
Ridhwan kutaka nieleze elimu yangu. WanaCCM walianza suala hili kwa ari,
nguvu na kasi mpya niliposema kwamba nchi imefika hapa ilipo kwa sababu
ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na upuuzi wa CCM.
Nikapuuza, naona sasa limeibuka tena kwa ari, nguvu na kasi zaidi baada
ya yaliyojiri bungeni kuhusu hoja binafsi niliyowasilisha bungeni kuhusu
maji na mkutano wa hadhara wa tarehe 10 Februari 2013 na masuala ambayo
niliipa Serikali wiki mbili kuyatolea majibu ama sivyo nitaongoza
maandamano ya wananchi kwenda Wizara ya Maji kutaka uwajibikaji na hatua
za haraka.
Kwa mara nyingine tena zinafanyika jitihada za kuhamisha wananchi kwenye
mjadala kwa kumshambulia mtoa hoja badala ya hoja, sasa ili turejee
kwenye mijadala ya msingi ni muhimu niweke kumbukumbu sawa kuhusu
masuala kadhaa kama yalivyoombwa.
Elimu yangu sio siri, nimegombea ubunge mara mbili mwaka 2005 na 2010 na
mara zote nimeeleza kuhusu suala hili; Nape na Ridhwan wangetumia tu
elimu yao wangetafuta kwenye mitandao na kukuta majibu wanayoyatafuta.
Nieleze kwa muktasari tu; nimesoma shule ya msingi Mbuyuni Dar Es Salaam
(nilikuwa mwanafunzi wa kwanza kwa mkoa wa Dar es Salaam).
Nilichaguliwa kwenda Shule ya Sekondari ya Ilboru wakati huo ikiwa ya
vipaji maalum, sikwenda; wito ulinituma kwenda Seminarini. Nilisoma
Franciscan Seminary Maua (FRASEMA) mpaka kidato cha nne; nilipata daraja
la kwanza; nikiwa na alama A katika masomo tisa.
Ningeweza kwenda shule yoyote ya Serikali ya kidato cha tano na sita
yenye mchepeo ambapo ningeutaka; lakini niliamua kubaki Dar es Salaam
shule ya Tambaza kwa sababu nilitaka kusoma huku nikiendelea na harakati
ambazo nilizianza kabla.
Hapa ndio ilikuwa chanzo cha mimi kuingia kwenye kazi ya kuhamasisha
mabadiliko kwenye mimbari nje ya utumishi wa madhabahuni. Tukio
lililobadili mwelekeo wa maisha yangu, mwaka 1998 nikiwa kidato cha nne;
nimesoma na tumeanza mitihani tukatangaziwa kwamba mitahani yote
imefutwa baada ya kuvujishwa.Tukarudishwa nyumbani kipindi hicho
nikaenda kwenye mafungo kujitafakari kwenye mkoa mmoja nikarejea Dar es
Salaam nikakutana na wanaharakati kadhaa wa asasi zisizo za kiserikali;
maelezo kuhusu ufisadi yalinifanya nione nina wajibu kwa nchi yangu,
nikarejea Seminarini kufanya mitihani nikiwa na fikra tofauti.
Matokeo yakatoka nimefanya vizuri, kwa mifumo yetu mibovu ya wakati huo
kwa mara ya pili tena Serikali hii inayoongozwa na CCM haikutambua
vipaji na nikapaswa niendelee kujilipia ada mwenyewe kama ilivyokuwa kwa
ngazi nyingine za elimu zilizotangulia; hapa nikakata shauri kwamba
nitatumia uwezo na uadilifu wote ambao Mwenyezi Mungu amenijalia
kuwezesha mabadiliko katika taifa letu.
Nikaamua kuacha kwenda kwenye shule za bweni mikoani na kubaki Dar es
salaam nisome Tambaza huku nikiendelea na kazi za harakati; wakati huo
nikihamasisha masuala ya ukombozi wa vijana nchini. Pamoja na kusoma
kutwa huku nikifanya kazi nilipata daraja la pili katika kidato cha
sita.
Taasisi nilizoanzisha au nilizoongoza katika kipindi hicho na kazi
nilizofanya sio siri na zinapaswa kujieleza zenyewe kwa matendo badala
ya maneno. Katika kipindi hicho, wakati huo kukiwa hakuna Mfuko wa Elimu
wala Bodi ya Mikopo nikashiriki katika ushawishi wa mabadiliko ya
kimfumo; nilikwenda Dodoma, tukakutana na wabunge na mawaziri
nikawasilisha mada “Towards a more functional education in Tanzania”,
wakati huo nikiwa mwanafunzi wa Sekondari.
Kati ya wabunge waliosikiliza mada niliyoiwaisilisha wakati huo sasa ni
Rais Jakaya Kikwete ( Ridhwan ukiwa nyumbani unaweza kumwuliza maoni
yake aliyotoa siku hiyo kuhusu ugharamiaji wa elimu na suala la mauaji
ya mwanafunzi wa Iyunga Michael Sikupya). Nilipotoka kwenye mkutano ule
Dodoma mwishoni wa miaka ya tisini, nilikata shauri kwamba mwaka 2005
nitagombea Ubunge hii ni baada ya kushudia aina ya wabunge waliokuwepo.
Mwaka 2002 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Es Salaam kusomea
“Bachelor in Business Administration (BBA) kwenye programu ya jioni;
nilifanya hivyo kwa kuamua kwa kuwa nilitaka nisome huku nikiendelea na
kazi. Mkuu wa Programu hiyo wakati huo alishangaa sana kwa umri wangu
(wakati huo shahada hiyo walikuwa wakisoma wazee watu wazima
wafanyakazi) na matokeo yangu (kwa kuwa yaliniruhusu kwenda kuingia
kusoma katika mfumo wa kawaida). Nikamweleza akanielewa kwamba sitaki
kusoma kama wanachuo wengine wa kawaida, uamuzi wangu huo ulikuwa na
gharama kwa kuwatafsiri yake ni kuwa nilipaswa kujisomesha binafsi.
Kwa hiyo mimi ni kati ya wale ambao hatudaiwi na nchi hii kwa maana ya
kwamba sijawahi kuchukua ruzuku wala kusomeshwa na Serikali hii
inayoongozwa na CCM; nimesoma kwa jasho la wazazi wangu na langu
binafsi. Kwa hiyo, nijibu tu kuhusu elimu yangu ya juu kwamba nimesoma
miaka mitatu Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (mtu aliyosoma kwa kiwango
hicho kwenye baadhi ya vyuo duniani hupewa associate degree).
Mwaka 2004 ikaanza misukosuko mbalimbali, mwaka huo ulikuwa ndio
unatungwa muswada wa Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, haya
matatizo yanayotokea leo niliyatabiri wakati huo. Niliwasilisha mada kwa
wanachuo kwenye ukumbi wa Nkurumah kuchambua udhaifu wa muswada huo na
kupata maoni ya wanafunzi kuhusu marekebisho yanayohitajika; wanachuo
wakapitisha azimio la kwamba muswada huo upingwe.
Kesho yake nikiwa Morogoro kikazi kukafanyika mgomo hatimaye wanafunzi
wakapigwa na kukamatwa.Nakumbuka nilikatiza kazi niliyokuwa nafanya
nikarejea kwa kuwa Chuo kiliweka sharti kwamba lazima wanachuo waache
mgomo ndio waliokamatwa waachiwe. Wakati huo Serikali ya wanafunzi
ilikuwa haisikilizwi, mimi na wengine wachache tukajitolea kuzunguka
kampasi na hosteli zote kushawishi wanafunzi kurejea masomoni na
wakafanya hivyo.
Serikali ya CCM ikatoa maelekezo kwamba kama tumeweza kuwafanya
wanafunzi warudi, hata kama sikushiriki mgomo na sihusiki na masuala ya
mikopo kwa kuwa ni mwanafunzi ninayejilipia mwenyewe lazima
nisimamishwe; nikiwa mwanafunzi pekee wa BBA niliyesimamishwa wakati
huo.
Nikarejea baada ya muda tayari kukiwa na mvutano kati yangu na utawala,
mwaka 2005 nikaamua kugombea Ubunge wakati huo nikiwa mwanafunzi;
mvutano ukaongezeka zaidi. Na utawala wa Chuo ukawa unapata mashinikizo
mengi kutoka kwa Serikali na CCM; wengine wakipendekeza nifukuzwe,
wengine nifelishwe na wengine nisiruhusiwe kuingia katika maeneo ya Chuo
jioni masomoni kwa kuwa nitakuwa nafanya kampeni.
Nikawa katika mtanziko(dilemma) wa kuchagua ama kuendelea na masomo na
kujitoa au kupunguza nguvu kwenye kampeni (mbinu nyingi zilitumika
wakati huo, sio sehemu ya majibu yangu ya leo) au niendelee na kampeni.
Nafsi yangu ikanituma kuamua kuandika barua yakuahirisha masomo, baada
ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005 mazingira yalikuwa yamebadilika
sana kuweza kurejea kumalizia mwaka au miezi michache iliyokuwa imebaki.
Mwaka 2006 nikiwa Marekani nilitafakari sana na kufikia uamuzi wa
kuendelea na kazi hii ya kusimamia mabadiliko na kujiandaa na uchaguzi
wa mwaka 2010. Mwaka 2010 niligombea tena na kushinda wakati huo huo
nikiongoza kazi za kitaifa za kampeni makao makuu pamoja na Profesa
Baregu na wengine; hakuna mahali popote nilipowadanganya wananchi kuhusu
elimu yangu, kama nilivyoeleza hapo juu.
Naamini wananchi wa Jimbo la Ubungo walinichagua kwa uwezo na uadilifu
wangu, na walijua pia kwamba nilikuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa
miaka mitatu. Naamini elimu ni kitu muhimu sana kwa kiongozi, lakini
wapo wenye elimu kubwa ya vyeti lakini hawajaelimika na wapo wenye elimu
ndogo sana ya vyeti lakini wanaelewa mkubwa wa kutimiza majukumu yao ya
uongozi.
Tangu mwaka 2012 na 2013, nimekuwa kwenye mtanziko mwingine na viongozi
wangu ndani ya chama wanafahamu; niliomba kuachia majukumu mengine yote
katika chama ili nibaki na ubunge peke yake niweze kuwatumikia wananchi
wakati huo huo niendelee na masomo zaidi ya elimu ya juu katika fani
inayoendana na kazi ninayoifanya ya sasa na matarajio yangu ya baadaye.
Hata hivyo, kwa mwelekeo huu wa Serikali na CCM leo nieleze tu kwamba
nikifanya hivyo itakuwa faida zaidi kwa watawala tunapoelekea mwaka
2015; hivyo, nimeamua kama nilivyoamua mwaka 2005; kwamba nitarejea
masomoni baada ya CCM kuondoka madarakani na Tanzania kupata Serikali
mpya itakayoongozwa na CHADEMA. Kwa sasa nitaendelea kujisomea kila
siku ninapopata wasaa kwa kuwa elimu haina mwisho.
Wakili Ridhwan katika maandiko yake amefanya rejea ya suala Kihiyo wa
CCM Temeke, nashauri arejee kwenye hukumu ya kesi ile na marekebisho ya
sheria yaliyofanywa na Serikali yaCCM kuwalinda wabunge wake vihiyo
baada ya hukumu.
Mifano hailingani kwa sababu mimi sijatoa maelezo ya uongo popote.
Lakini hata kwa wabunge wa CCM wanaotoa maelezo ya uongo wa wapiga kura,
marekebisho hayo yamewawekea wigo wa mianya yakutokea mahakamani.
Zamani fomu zakuogembea zilikuwa na mahali pa kujaza elimu ya mgombea,
sasa kipengele hicho kimeondolewa. Hivyo, suala la kughushi na kutoa
taarifa za uongo haliko kama ilivyokuwa awali, isipokuwa kesi inaweza
kufunguliwa ya ukiukwaji wa kawaida wataratibu za kampeni kwa
kuwashawishi wapiga kura kwa taarifa za uongo (ndani ya ule muda wa
kisheria wa kesi kufunguliwa ambao ulishapita).
Halafu ni jukumu la mlalamikaji sio tu kuthibitisha kwamba uongo
ulitolewa bali uongo umeathiri vipi matokeo. Ndio maana leo kuna vihiyo
wengi tu wa CCM ndani ya Bunge lakini ni vigumu kuwabana kwa mfumo wetu
wa sasa. Baada ya majibu hayo marefu, naamini sasa Nape unaweza sasa
kurejea kwenye kujibu; Elimu ya Mnyika ina uhusiano gani na CCM kuahidi
kwenye ilani yake na kushindwa kutekeleza kwamba ifikapo mwaka 2010
asilimia 90 ya wananchi wa mijini ikiwemo Dar essalaam watakuwa wanapata
maji safi na salama? Ridhwan kwa kuwa umeweza kufanya rejea unaweza pia
kueleza ni kwanini Rais Kikwete mwaka 2011 aliahidi kuwa tatizo la maji
Dar es Salaam litakuwa historia mwezi Februari 2013 lakini mwezi huo
umefika na matatizo bado ni makubwa?

By Ridhiwan Kikwete
NIMEKUELEWA MBUNGE WANGU MNYIKA
Nimeisoma vizuri taarifa ya bwana Mnyika na nimeielewa. Nimeona sababu
za msingi kwanini hakumaliza shule na majibu juu ya hoja ambayo
aliisimamisha bwana Nape Nnauye.
Ni jambo zuri ambalo amelifanya maana tumefunguka na kujua ukweli. Lakini naomba radhi kama sikueleweka vizuri.
Nilichofanya mie ni kumuita ukumbini ili atutoe wasiwasi hasa mimi kama
nilivyojielewa kuwa nilikuwa naye chuoni na ninaheshimu sana uwezo wake
wa ufahamu.
Mwisho nimuhakikishie, ni jukumu la CCM kuhakikisha kuwa maji
yanapatikana Jimboni Ubungo na tutayaleta. Kubwa zaidi akumbuke ilani
yetu ni ya miaka mitano na maji yatafika pale kabla ya 2015.
La msingi aendelee kuisukuma serikali na kumkumbusha waziri Maghembe juu
ya utekelezaji wa ya maneno yake mazuri na sio mbwembwe za kufurahisha
baraza.
Mwisho, nikupongeze mnyika kwa kuja hadharani na kutoa wingu. Ni imani bwana Nape na wasomaji wengine tumekuelewa.
Shukrani. Hatuchafuani, tunasaidia kuwekana sawa . Huu ndiyo uwazi kwa vitendo. Hongera muheshimiwa mbunge wangu.
Chanzo Jamii Forum
Post a Comment