CHINA imeahidi kuleta nchini watalii 30,000 katika kipindi cha miaka
mitatu kuanzia mwakani.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Wakala wa kutoa huduma za
usafiri wa China na Hong Kong, Zhang Xuewu alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda jijini Shenzen, China.
Alisema kampuni yake itawandaa mawakala wa usafirishaji watalii kuhakikisha
kuwa watalii 10,000 wanapatikana kila mwaka ambao kiu yao ni kuja nchini.
“Wengi wanapenda kutembelea mbuga, lakini hapa nchini wamezoea kuona
walio sakafuni, wakija watawaona wanyama live” (akimaanisha kuwa Wachina
wamezoea kuona wanyama wa sanamu kwenye makumbusho yao hapa jiji la Shenzhen).
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi ya
siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya China, alisema haelewi ni kwa nini kampuni
hiyo imeweza kupeleka watalii Afrika Kusini na nchi jirani za Afrika Mashariki
wakati haina urafiki nazo lakini imeshindwa kuwaleta Tanzania yenye uhusiano
mzuri kwa muda mrefu.
Akizungumza na Xuewu pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania
alioambatana nao, Waziri Mkuu alisema amepewa maelekezo rasmi na Rais Jakaya
Kikwete ya kufuatilia suala la watalii wa kutoka China, hasa ikizingatiwa
kwamba mazungumzo ya jambo hili yalianza wakati wa Rais wa awamu ya tatu,
Benjamin Mkapa.
“Katika bara la Afrika hakuna nchi yenye vivutio lukuki kama Tanzania.
Na tovuti ya www.safaribooking. com imeitangaza Tanzania kuwa nchi inayofaa kwa
safari za mbugani kama mtu anataka kuona vivutio vizuri na vya asili. Sasa ni
kwa nini hatupati watalii wa kutosha na tunafanyaje ili kubadilisha hali hiyo?”
alihoji.
Alisema njia mojawapo ni kuhakikisha kunakuwa na ndege ya moja moja
kutoka miji ya China hadi Dar es Salaam, jambo alisema litasaidia kupunguza
kero kwa wasafiri ambao hivi sasa inabidi waunge safari mara mbili hadi tatu
ili kufika Tanzania.
“Tuangalie uwezekano wa kuwa na ndege ya moja kwa moja kutoka China hadi
Dar es Salaam au Arusha... wenzetu Kenya na Afrika Kusini wameweza kupata
watalii wengi sababu wana ndege za moja kwa moja,” alisema.
Alimshawishi mwenyekiti huyo aangalie pia uwezekano wa kujenga hoteli
katika mikoa nchini kupunguza uhaba wa vyumba punde watalii wakianza kufurika.
Pia alimhakikishia fursa ya kujenga uwanja wa gofu chini ya mlima
Kilimanjaro kwani yote mawili ni maeneo ambayo kampuni yake inao uwezo wa
kufanya kama sehemu ya majukumu yake.
Post a Comment