Home » , » Wawakilishi Zanzibar wakataa taarifa ya Serikali

Wawakilishi Zanzibar wakataa taarifa ya Serikali

Written By peterdafi.blogspot.com on Sunday, October 20, 2013 | 10:26 PM

BLW

Zanzibar. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameikataa taarifa ya Serikali jinsi ilivyolishughulikia sakata la ubadhirifu unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji katika Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) visiwani humu.

Msimamo huo wameutoa wakati wakichangia taarifa iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar kinachoendelea huko Chukwani mjini Unguja.

Mwakilishi wa Mkwajuni Mbarouk Mussa Wadi (CCM) alisema kwamba Serikali haijachukua hatua yoyote dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuliibia shirika na badala yake imewalinda ikiwemo kuwahamisha ofisi na wengine kuwapa onyo Meneja Mkuu na wasaidizi wake Pemba.

Wadi alisema kwamba kitendo kilichofanywa na Serikali ni sawa na dharau dhidi ya Baraza la Wawakilishi kwa vile Serikali imeonyeshwa kutotekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Fedha ya Baraza la Wawakilishi (PAC) ikiwemo kuchukuliwa hatua za kisheria watu waliohusika na ubadhirifu huo.

Alisema kamati ya PAC ilipendekeza ufanyike ukaguzi maalumu ndani ya shirika hilo na kazi hiyo ifanywe na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kupitia mapato na matumizi ya kuanzia mwaka 2009 hadi 2012, kazi ambayo haijafanyika kwa zaidi ya miezi saba tangu kutolewa kwa mapendekezo hayo.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Ali Salum Haji alisema kwamba kifungu cha 84 cha kanuni za utumishi serikalini kinaeleza kuwa mfanyakazi anapokabiliwa na tuhuma za ubadhirifu au wizi hutakiwa kusimamishwa kazi na kufunguliwa mashtaka na si kuhamishwa kutoka ofisi moja kwenda nyingine au adhabu ya onyo. Mwakilishi wa Kiwani, Hija Hassan Hija alisema umefika wakati Baraza la Wawakilishi lisiunde tena kamati teule za uchunguzi kwa vile Serikali haitaki kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na Baraza hilo.

Hija alisema tayari kuna ripoti nne za kamati teule ambazo hazijatekelezwa hadi sasa ikiwemo ile ya uchunguzi wa uuzaji wa majengo ya umma ya Mambo Msiiige, ubadhirifu unaodaiwa kufanyika katika Baraza la Manispaa ya Zanzibar, ukodishwaji wa kisiwa cha Changuu, ubadhirifu wa shirika la Zeco na ununuzi wa mali za Serikali bila ya kuzingatia sheria ya ununuzi. “Serikali ni dhahiri inawaogopa watendaji wake au inakusudia kuficha dhambi za wakubwa kuliko za watendaji, umefika wakati Baraza likatae kuunda kamati za uchunguzi, hakuna faida kwa wajumbe pia kwa wananchi waliowachagua wawakilishi wao,” alisema Hija.

Hata hivyo, alisema kwamba huu ni wakati mwafaka kwa wawakilishi kuwaeleza washirika wa maendeleo wanaochangia fedha za maendeleo kuwa hazijainufaisha Zanzibar na wananchi wake kutokana na vitendo vya ufisadi vinavyojitokeza na wahusika kutochukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin, alisema jukumu la kikatiba la Baraza la Wawakilishi la kuisimamia Serikali limepotea kutokana na kuwakingia kifua mafisadi na kusababisha ripoti za Baraza za uchunguzi kubakia kama boya na wahusika kutochukuliwa hatua za kisheria.

Salim alisema BLW kuendeleza kuunda kamati za kuchungua ubadhirifu bila ya wahusika kuchukuliwa hatua kunaendelea kulishushia hadhi Baraza hilo na kumtaka Spika kutounda tena kamati hizo kwa vile hutumia fedha za walipakodi bila ya matunda yake kuonekana.
Alisema taarifa ya Serikali ililidanganya Baraza kutoa mfano katika ripoti ya uchunguzi wa fedha kuwa mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar awamu ya sita Shumbana Amani Karume aliundiwa umeme na kutumika nguzo zaidi ya 40 bila ya malipo, lakini taarifa ya Serikali imesema ni nguzo 20 kinyume na ukweli ulivyo.

“Ushahidi wa madai hayo upo, hakuna vielelezo vyovyote vikionyesha malipo alioyafanya, taarifa ya Serikali siiungi mkono, haina ukweli na hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa ubadhirifu,” alisema Salmin

Kwa hisani ya Mzalendo net, Zanzibar Kwanza

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger