Home »
kitaifa
,
siasa
» Nzega: Tumefika Wapi Leo? Tunaelekea Wapi Kesho? Taarifa ya Ofisi ya Mbunge Kufunga Mwaka 2013
Nzega: Tumefika Wapi Leo? Tunaelekea Wapi Kesho? Taarifa ya Ofisi ya Mbunge Kufunga Mwaka 2013
Nzega: Tumefika Wapi Leo? Tunaelekea Wapi Kesho? Taarifa ya Ofisi ya Mbunge Kufunga Mwaka 2013.
Utangulizi
Ukiitazama Nzega ya leo si ile Nzega ya Miaka ya 90 ama ile ya miaka ya
70, alipozaliwa Mbunge wetu Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.), imebadilika
sana, imekuwa kwa kasi sana; idadi ya watu, magari na nyumba imeongezeka
sana. Utoaji wa huduma zote muhimu umezidiwa kasi na ukuaji wa mji.
Changamoto zilizopo leo ni nyingi na nzito sana. Kuna shida kubwa ya
upatikanaji wa maji safi na salama, shule ni chache na zinatoa elimu
isiyokidhi ubora unaohitajika, viwanda hakuna ukilinganisha na miaka ya
nyuma, migodi midogo midogo iliyokuwa asili ya Nzega imefungwa na
serikali, mvua zimepungua kutokana na uharibifu wa mazingira hivyo
uzalishaji wa mazao ya biashara na kilimo umeathiriwa sana ukilinganisha
na miaka ya nyuma, miundombinu ya barabara imeongezeka kwa wingi haswa
maeneo ya vijijini na mijini japokuwa bado ni duni na haitoshi na pia
huduma za kibenki ni duni na hazijawafikia wananchi walio wengi kule
vijijini.
Pamoja na mapungufu haya Nzega inafaidika kwa kuwa
kwenye nafasi nzuri kijiografia, kwamba ni makutano ya barabara kuu
ziendazo Kigoma, Kagera hadi Rwanda na Burundi na ile inayokatiza kwenda
Mwanza hadi Musoma na Tabora hadi Mbeya. Kama zikiunganishwa kwa lami,
Nzega inaweza kuwa kituo muhimu kwa biashara. Pia nafasi yake
kijiografia imefanya Nzega iwe na mchanganyiko mzuri wa watu kimakabila
kiasi kwamba mchanganyiko huu unatoa fursa ya kuleta uzoefu na ujuzi
mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali ambao unapafanya Nzega pawe mahala
palipochangamka (vibrant and dynamic).
Mwaka 2010, kwenye
uchaguzi Mkuu, Nzega ilifanya uamuzi sahihi wa kumchagua Mbunge
mwanamapinduzi, mwanamabadiliko na mpiganaji mahiri na makini, Dkt.
Hamisi Kigwangalla (Mb.) ambaye anajitahidi kupambana na changamoto hizi
usiku na mchana pasi na kukata tamaa ama kuchoka. Mafanikio ya kazi
yake yanaonekana na siyo ya kutafuta. Ifuatayo ni ripoti ya utekelezaji
wa majukumu ya Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) hadi
kufikia Desemba 2013.
1. Hali ya Jimbo
Hali ya jimbo
ni shwari; amani, upendo na usalama umetamalaki japokuwa mpaka
tunaandika taarifa hii kuna malalamiko ya watu wa kijiji cha Mwanshina,
ambako kuligundulika uwepo wa dhahabu hivi siku za karibuni na kupelekea
wananchi kujumuika pale kuanza shughuli za uchimbaji; bahati mbaya sana
wamezuiliwa na askari wa kutuliza ghasia (FFU) waliopokea maelekezo
kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega. Mazungumzo yanaendelea kujua ni kwa
nini serikali imewazuia wananchi hawa ili hatma ya mgodi huu ijulikane.
Pili, kuna malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Ipala ambao wanadaiwa na
serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega kuvamia eneo la msitu
wa hifadhi. Ufuatiliaji wa uhalali wa katazo la Mkuu wa Wilaya ya Nzega
lililoambatana na uvunjifu mkubwa wa haki za wananchi, ambapo wamedumu
toka kabla ya uhuru, unaendelea.
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega
imeendelea kuhudhuria shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo harusi,
misiba, mahafali za wanafunzi, harambee na pia kufanya ziara za kikazi
kijiji kwa kijiji kupitia ‘Operesheni Wafuate Watu’. Pia ahadi za Mbunge
ama wasaidizi wake kwenye maeneo mbali mbali zimekuwa zikitekelezwa –
hadi sasa ni zaidi ya asilimia 95 ya ahadi zote alizotoa mbunge
zimetekelezwa ukiachilia chache sana ambazo ni za siku za karibuni. Kuna
ligi kubwa ya kiwilaya inayofadhiliwa na Mbunge wa Nzega inaendelea
katika hatua ya robo-fainali kwenye tarafa nne za Wilaya ya Nzega –
mshindi wa kwanza atapata ‘Kombe la Kigwangalla’ na fedha taslim TZS
1,000,000, wa pili atapata TZS 500,000 na wa tatu TZS 300,000. Timu zote
zilizoingia nane bora zitazawadiwa seti moja ya jezi kila timu.
Mbunge wa Nzega anaendelea kupigana kuhakikisha azimio la Baraza la
Madiwani la kuanzisha Kampuni ya Benki Jamii ya Nzega (Nzega Community
Bank Ltd - NCB) na Kampuni ya Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community
Construction Corporation Ltd - NCCCL) linatekelezwa haraka. Tunatarajia
mchakato huu utafanikiwa kutokana na uwepo wa takriban TZS 2.3 bilioni
zilizopatikana kutoka kampuni ya Resolute Tanzania Ltd kama ushuru wa
huduma (service levy) na ambazo zitatumika kama mtaji wa kuanzia wa
benki (TZS bilioni 1) na zinazobaki kwa ajili ya kununulia mashine za
kuchongea barabara na kuchimbia visima zitakazomilikiwa na kuendeshwa na
kampuni hizi mbili tofauti ambazo zinatarajiwa kuanzishwa kwa
ushirikiano baina ya Halmashauri, wanaushirika na wananchi wengine
watakaopenda kununua sehemu ya hisa za makampuni haya mawili.
2. Vipaumbele Vya Jimbo
2.1 Mapinduzi Kwenye Sekta ya Elimu Nzega:
(i.) Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, mpaka sasa kwa kufanya
jitihada binafsi na kwa kutumia pesa za mfuko wa jimbo (milioni 43)
akishirikiana na Diwani, Mhe. Ramadhani Nchimani, Kamati ya Maendeleo ya
Kata ya Ndala, Serikali ya Kijiji cha Kampala na wananchi kwa ujumla,
ameanzisha ujenzi wa shule mpya ya ‘high school’ (kidato cha tano na cha
sita) pale Kampala, Ndala (Shule hii imepewa jina la Chief Ngelengi
High School); ujenzi unaendelea kwa kasi hivi sasa. Shule ya pili ya
High School itakuwa ni ile ya Chief Ntinginya, ambapo Mbunge wa Nzega
Dkt. Hamisi Kigwangalla, kufuatia makubaliano na Kamati ya Maendeleo ya
Kata ya Nzega Mjini chini ya Diwani na Mwenyekiti wake Mhe. Kizwalo
Dominic waliazimia kuanzisha ujenzi wa mabweni na madarasa ya ziada ili
kuipandisha hadhi shule hii iwe ya kidato cha tani na cha sita. Shule ya
tatu ya High School inamaliziwa kujengwa Kata ya Puge, Tarafa ya Puge
kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mbunge (ambayo imetoa sh milioni 13), Diwani
Mhe. Alex Nyassani, Serikali ya Kijiji cha Upungu na wananchi kwa
ujumla (ambao walianzisha majengo hayo); pia Halmashauri ya Wilaya
tayari, kwa ushawishi wa Mbunge wa Nzega na Diwani wa Kata ya Puge,
imetenga fedha taslimu sh milioni 28 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa
shule hiyo. Shule ya Nne ya High School inamaliziwa kujengwa kule Kata
ya Lusu (pale Hamza Azizi Ali Sekondari) na wawekezaji wa mgodi, Kampuni
ya Resolute Tanzania Ltd, kufuatia jitihada za kiufuatiliaji na
ushawishi wa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) na Mhe. Said Mgalula
(Diwani, Lusu) wakishirikiana na wananchi, kwamba ni lazima mgodi ujenge
miradi ya maendeleo ya jamii kabla haujafungwa. Ni matarajio yetu
kwamba shule hizi zitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi kabla ya
mwaka 2014 kuisha. Tunawaomba wananchi wote kwa ujumla, wadau mbalimbali
wa maendeleo na serikali tutimize wajibu wetu, tumuunge mkono Mbunge
wetu tulete mapinduzi ya kielimu Nzega.
(ii.) Mbunge wa
Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na shirika lisilo la
kiserikali la PeerCorps Trust Fund ameweza kuanzisha mpango wa kusomesha
watoto yatima na wanaotoka familia zenye kipato duni, mfuko huu
unaoitwa Hamisi Kigwangalla Scholarship Fund ulianzishwa mwaka 2008 na
umeendelea kusomesha watoto na kutoa misaada mbalimbali ya kielimu.
Mpaka sasa zaidi ya watoto 576 wamefaidika na mpango huu. Na kila kata
kuna wanafunzi 10 kutoka katika makundi haya wanalipiwa ada chini ya
mpango huu. Japokuwa mfuko unakumbana na changamoto nyingi ikiwemo
kupata maombi mengi zaidi ya uwezo wa mfuko na kuna baadhi ya kata mpaka
sasa mfuko haujaweza kupata fedha za kulipa ada kwa baadhi ya
wanafunzi, japokuwa Mhe. Mbunge anawataka walimu, wazazi/walezi na
viongozi wa Kata hizo wawe wavumilivu na kwamba ada hizo zitalipwa kabla
watoto hao hawajahitimu kwa kuwa majina yao tunayo na yaliishapitishwa
kufaidika na mpango huu.
(iii.) Mwezi Januari mwaka 2014
Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, atauanza mwaka kwa kuendelea
kugawa vitabu 100 vya Kiada na 50 vya ziada kwenye shule zote za
Sekondari za Kata za Jimbo la Nzega pamoja na Kompyuta kwenye shule 5 za
sekondari kama ambavyo amekuwa akifanya toka achaguliwe kuwa Mbunge wa
jimbo hili.
(iv.) Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla,
ameanzisha tamasha la utamaduni wa watu wa Nzega litakalokuwa
likifanyika kila mwaka mjini Nzega. Tamasha hilo ambalo linaitwa Mtukwao
Festival (www.mtukwao.org)
litakuwa ni kivutio cha watu na kuleta fursa ya biashara kwa wakazi wa
Nzega, na sehemu ya kuitangaza Nzega na utamaduni wake kwa wageni,
tayari limepata usajili wa serikali na maandalizi yanafanyika kulizindua
mnamo Julai 2014 kwa mara ya kwanza, baada ya mipango ya kulizindua
Julai 2013 kama ilivyotangazwa hapo awali kushindikana.
(v.)
Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha ujenzi wa chuo
binafsi mjini Nzega eneo la Uchama kitakachokuwa kinatoa wahitimu kwenye
fani za Uganga, Uuguzi na Ualimu kwa ngazi za Vyeti na Stashahada ili
kuongeza nguvu kazi kwenye shule za sekondari za kata, zahanati na vituo
vya afya. Malengo ni kusomesha bure walau wanafunzi watano - kwenye
kila kozi, wasio na uwezo, mbali na wale wanaojilipia, kwa makubaliano
ya kuhakikisha wanaajiriwa kwenye wilaya ya Nzega kwa kipindi
kisichopungua miaka mitano. Hii itaongeza idadi ya watumishi kwenye
huduma muhimu kwa wananchi na pia uwepo wa chuo utakuza fursa za
kiuchumi na ukuaji wa taswira ya mji wa Nzega. Tunatarajia chuo hiki
kitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi mwaka 2014 Mwezi Septemba.
2.2 Kuendesha Harakati za Kupigania Haki na Usawa kwa wanaNzega: Mbunge
wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na wananchi wa
Nzega, madiwani na watendaji wa halmashauri ameongoza mapambano ya kudai
haki za Nzega dhidi ya wawekezaji wa Mgodi wa Golden Pride Project,
kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, na kufanikiwa kupata mafanikio
yafuatayo: mgodi umekubali na tayari umelipa sh bilioni 2.34 kama ushuru
wa huduma (service levy) kwa halmashauri ya wilaya ya Nzega, bado kuna
madai ya sh bilioni 4 za ushuru wa huduma yanayoendelea kufuatiliwa,
ambazo ni malimbikizo ya ushuru huo toka mgodi uanzishwe takriban miaka
14 iliyopita; amefanikiwa kuishawishi serikali kuwa wananchi waliopoteza
mali zao kutokana na uharibifu uliofanywa kupisha mgodi wana haki ya
kifuta jasho na sasa serikali inaungana na Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla
kuwabana wawekezaji waanzishe mfuko wa kuwahifadhi wananchi hao; na
jambo kubwa la tatu ni kwa kutumia nguvu ya umma kushawishi wawekezaji
watekeleze ahadi za kujenga miradi ya maendeleo Nzega (Kituo cha Afya
Lusu, Maabara kwenye sekondari 10 n.k.). Mbunge wa Nzega ataendelea
kushawishi vikao vya halmashauri na kusimamia utekelezaji wa miradi
itakayowagusa wanaNzega wengi zaidi, kama vile kuanzisha benki ya jamii
ya watu wa Nzega ambayo itatoa mikopo kwenye SACCOS za kila kata,
kununua mitambo yetu wenyewe ya kuchimbia visima kwenye kila kijiji,
kujenga soko jipya na stendi mpya kubwa ili kukuza fursa za biashara
ndogondogo kwa wananchi n.k. Mhe. Mbunge amekuwa akipigana bega kwa bega
na wananchi wa Kijiji cha Mwabangu kuhakikisha wanapata haki ya
kupatiwa leseni yao iliyopokwa kinyemela na wajanja wachache kwa faida
yao ama fidia ya ardhi ya mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo wa
Isungangwanda.
2.3 Kuwezesha Wananchi Kushiriki Shughuli
Mbalimbali za Kukuza Kipato Chao: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi
Kigwangalla, amefanikiwa kuleta mapinduzi ya kijani kwenye kilimo cha
zao la pamba na zao la alizeti kupitia uhamasishaji wa kampuni ya MSK
Solutions Ltd ambayo inatoa mbegu bora, pembejeo, zana za kilimo, elimu
ya kilimo bora na uwezeshaji wa wagani vijijini, soko la uhakika la
mazao hayo na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao vijijini
(Imekamilisha ujenzi wa maghala kule Ndekeli (Tarafa ya Puge), Igalula
(Tarafa ya Mwakalundi), Nhabala (Tarafa ya Bukene) na imeanza ujenzi wa
ma-godown mapya kule Nhobola (Tarafa ya Nyasa) na Usongohala (Tarafa ya
Bukene). Mafanikio ni kuongezeka kwa wakulima wa pamba kutokea wakulima
355 mwaka 2008 hadi kufikia wakulima 24,000 wa pamba mwaka 2012 na
kufanya idadi ya kilo za pamba zilizovunwa kufikia takriban milioni 6
kutoka kilo 20,000 mwaka 2008. Pia idadi ya wakulima wa alizeti
imeongezeka kutoka wakulima 400 mwaka jana hadi kufikia 3500 mwaka 2013.
Makampuni ya wanunuzi wa pamba yameongezeka kutoka kampuni
moja ya MSK na kuwa manne hivi sasa – hali inayoleta ushindani kwenye
soko na hivyo kupandisha bei zaidi kwa faida ya mkulima. Japokuwa
kampuni ya MSK Solutions Ltd imeamua kuacha kuhamasisha pamba na
kujikita zaidi kwenye alizeti itaendelea kukumbukwa kwa kutia chachu
uhuishaji wa kilimo cha zao hili kilichokuwa kimekufa.
Mipango
inaendelea kuwashawishi wawekezaji wajenge viwanda vya kuchambua pamba
na kukamua mafuta ya kula kutokana na alizeti ya Nzega, tayari
halmashauri ya Nzega imeazimia kutenga viwanja 10 kwenye eneo maalum la
kujenga viwanda. Pia Mbunge wa Nzega amewezesha wananchi kujiunga katika
vikundi vya ushirika wa SACCOS vipatavyo 9 na yupo kwenye harakati za
kuvijengea uwezo vifanye kazi za kukuza uchumi kama vile kilimo, mifugo
ya kuku kwa kuzalisha vifaranga na mayai, na shughuli za ufundi kwa
vijana. Mbunge wa Nzega amegawa mashine mbili kwenye SACCOS ya vijana
nay a wazee kwa ajili ya kuangulia vifaranga. Ili kuhakikisha chama
kinakuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za
maendeleo vijijini, Mbunge wa Nzega akishirikiana na mwenzake wa Bukene
wamegawa mbegu za alizeti kwenye kila kata. Pia Mbunge wa Nzega amegawa
pikipiki 10 kwenye kata 10 ili kuweka urahisi zaidi wa kufikisha huduma
za ushauri wa maendeleo kwa wakulima vijijini.
2.4 Ujenzi wa
Miundombinu Nzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla,
ameweza kushawishi vikao mbalimbali vya maamuzi na kuhakikisha azimio la
kujenga barabara za lami Nzega Mjini linafanikiwa, hivi sasa tayari
bajeti imetengwa kwa ajili ya kutekeleza hilo kwenye mwaka wa fedha wa
2013/14; pia kufunga mataa ya kuangaza mji mzima wa Nzega. Mbunge wa
Nzega pia kupitia mfuko wa Jimbo amejenga daraja korofi na
lililosahaulika kwa muda mrefu la Butandula, na sasa anatafuta namna ya
kuhakikisha pia daraja lingine la Nhobola nalo linajengwa, tayari
ametenga sh milioni 8 za mfuko wa jimbo kutekeleza hilo.
Mradi
wa barabara ya Nzega – Tabora kwa kiwango cha lami – Mbunge wa Nzega
kwa kutumia nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya
Mkoa wa Tabora, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha serikali inaleta
fedha za kukamilisha mradi huu ndani ya muda uliopangwa na pia kusimamia
kuhakikisha barabara hiyo na nyingine za mkoa wa Tabora, zinajengwa kwa
viwango vya ubora unaostahiki, na wananchi wanapata ajira na kulipwa
fidia ya mali zitakazoathiriwa na utekelezaji wa mradi huu.
Pia Mbunge amehakikisha barabara korofi kama za kutoka Mbagwa –
Nkiniziwa, Busondo – Ndekeli, Busondo – Mwakashanhala zinaingia kwenye
bajeti ya ujenzi mwaka huu wa fedha 2013/14 na kuhakikisha zinajengwa,
pia barabara nyingine muhimu kama za Muhugi – Mizibaziba – Ndekeli –
Ndala zinaingizwa kwenye bajeti, lengo likiwa ni kuhakikisha Nzega
inakuwa na mtandao mzuri wa lami mahala pote. Mhe. Dkt. Hamisi
Kigwangalla (Mb.) amefanikiwa kuhakikisha mradi wa kupeleka umeme Ndala
kutoka Nzega unatekelezwa kwa viwango vya ubora unaofaa, na sasa
anahangaika kuhakikisha pia maeneo ya Mbogwe, Wela, Miguwa, na yale ya
Usagali, Kaloleni hadi Mirambo Itobo nayo yanapata mradi wa Umeme.
Tayari maombi yake yameingizwa kwenye orodha ya miradi ya Umeme Vijijini
(REA Phase II) na hivyo maandalizi ya awali ya upembuzi yakinifu
yataanza muda wowote kuanzia sasa. Sambamba na jitihada hizi, Mbunge
amefanikiwa kuishauri na hatimaye kuishawishi halmashauri ya Nzega
kuanzisha kampuni ya ujenzi (NCCCL) na kuinunulia mitambo ya kuchongea
barabara, mpango ambao upo kwenye hatua za utekelezaji.
2.5
Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Nzega: Baada ya kutoridhishwa na
namna miradi ya maji ya benki ya dunia na ile ya serikali inavyosuasua,
Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameshauri na hatimaye
kuishawishi Halmashauri wanunue mitambo ya kuchimba visima na kuiweka
chini ya usimamizi wa kampuni ya ujenzi Nzega (NCCCL) ili kuondoa yale
matatizo kwamba mkandarasi amelipwa achimbe kisima kimoja akikosa maji
basi na pesa ya serikali ndiyo imeishaliwa. Pesa za kununulia mitambo
hiyo zitatokana na mapato yaliyopatikana kutokana na ushuru wa huduma
uliolipwa na kampuni ya Resolute. Tukiwa na mitambo yetu tutahakikisha
tunachimba kisima na maji yanapatikana kwenye kila kijiji bila shida
ndipo twende kijiji kingine. Pia Mhe. Mbunge amekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja Mkoa wa Tabora
unaanza kutekelezwa – na kwa sasa hatua ya utafiti wa awali
ilishamalizika na tunatarajia upembuzi yakinifu utafanyika mwaka huu na
pengine mwakani kuanza kutekelezwa, ukizingatia hii ni ahadi ya Mhe.
Rais Dkt. Jakaya Kikwete.
2.6 Upatikanaji wa Huduma Bora za
Afya kwa Umma: Mhe. Mbunge, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameamua kuanzia
mwaka 2014 ataweka ratiba maalum ya kutumia taaluma yake ya udaktari
kutibu wagonjwa kwenye vituo mbali mbali vya afya Nzega. Pia ameandaa
mkakati kabambe wa kuleta madaktari bingwa wanaoruka (flying doctors)
kwa ajili ya kuweka kambi ya tiba maalum mara mbili kwa mwaka kwa ajili
ya wananchi wa Nzega. Kwa kushirikiana na madiwani wenzake wa
halmashauri ya Nzega wamefanikiwa kuhakikisha vituo pamoja na nyumba za
walimu zilizoanza kujengwa na wananchi vinamaliziwa chini ya Mpango wa
Maendeleo ya Afya ya Msingi – tayari bajeti imetengwa kumalizia vituo
vyote mwaka 2013/14, na anaendelea kuhamasisha vijiji vingine ambavyo
havijaanza kutekeleza mpango huu vianze mara moja ili tubaki tukitafuta
namna ya kupambana na chamngamoto nyingine za watumishi, vifaa na
madawa.
N.B: Kuna mambo mengi yanayofanyika Nzega kwa
ushawishi wa Mbunge na Madiwani, yakitekelezwa na serikali kutokana na
maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, mwaka 2010 – 2015, lakini si yote
yaliyoripotiwa hapa.
Taarifa hii imetolewa na Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega, pia inapatikana hapa www.hamisikigwangalla.com na http://kigwangalla.blogspot.com/
Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb.)
Leo Siku ya Jumamosi, Desemba 21, 2013.
Post a Comment