Wakati
taifa likielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, shehia, vijiji
na vitongoji, wanasiasa kadhaa wameshaanza safari ya kuwania Urais kwa
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.
Wapo waliowahi kugusia nia zao zinazowaongoza kuwania nafasi hiyo,
na wapo ambao hata sasa wanazungumza ‘kimtindo’, lakini walio wajanja,
wanatambua kwamba kinacholengwa katika michakato iliyopo, ni kuutaka
Urais.
Lakini wapo wanaotajwa, wakihusishwa na nia kama hiyo, hata kama
wenyewe hawajajitokeza hadharani na kuzungumzia suala hilo, achilia
mbali ‘kujipitisha pitisha’ kwa wapiga kura.
Mmoja wa wanasiasa miongoni mwa walio vijana, wanaotajwa kuwa
katika kinyang’anyiro hicho, ni Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi
Kigwangalla, anayetajwa zaidi kupitia mitandao ya kijamii na siasa za
ndani ya jimbo hilo lililopo mkoani Tabora.
Lakini katika mahojiano yake na safu hii juzi, Dk Kigwangalla,
pamoja na mambo mengine, akana kuwa hana nia ya kuwania nafasi hiyo ya
uongozi wa juu nchini, huku akiwakosoa wanaojitokeza hivi sasa katika
taswira ya ‘kuelekea Ikulu’
Sijawahi kutamka kwamba nitagombea ama ninautaka urais.
Ninawapongeza waliojitangaza ingawa sidhani kama ni sahihi kufanya hivyo
kwa wakati huu,” anasema.
Anasema, kujinadi miongoni mwa wanasiasa si dhambi, lakini kufanya
shughuli hiyo kabla muda haujafika ni kosa la kiutendaji kwa sababu
linaharibu utendaji mzima wa mtu ambaye ameshikilia nafasi hiyo.
“Sisi kwa mfano tuliogombea ubunge ama udiwani ama kwa Rais wetu,
tunajua kabisa muda tuliopewa kikatiba ni miaka mitano, na baada ya
miaka hii mitano, uongozi utabadilika, tunalifahamu hilo bila shaka
yoyote,” anasema.
“Lakini kwa leo hii mtu kuanza kufanya kampeni Januari 2014, ni
kuingilia utendaji kazi wa mbunge aliyepo madarakani, ama ni kuingilia
utyendaji kazi wa Rais aliyepo madarakani. Lakini pia ni kuwachanganya
wananchi na wanachama wa vyama vyetu kuanza kufanya kampeni mapema
kabla ya muda.”
Dk Kigwangalla anasema wananchi wanapaswa washiriki shughuli
nyingine za kimaendeleo zaidi ya kuwa kila siku wanatumikia matakwa ya
wanasiasa.
MIGOGORO NDANI YA VYAMA VYA SIASA
Dk Kigwangalla, anasema siasa ndio mustakabali wa taifa kwa sababu
ndani yake (siasa) wanapatikana viongozi wanaowaongoza wananchi katika
dira yenye kuleta maendeleo kwa wananchi.
Anatoa wito kwa wanaofuatilia ama kushabikia siasa, kutovuruga
amani ya taifa kutokana na mitazamo binafsi ya wanasiasa husika.
Hata hivyo, anakisifia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa uzoefu wa
kutatua migogoro na kudumisha amani na mshikamano ndani yake, jambo
ambalo kihistoria limekuwa likijitokeza na ambalo limekuwa likipatiwa
ufumbuzi bila shida.
“Bahati nzuri mimi ninatoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi, hata
tugombane namna gani mwisho wa siku huwa tunapatana, tunashikamana,”
anasema.
MAWAZIRI KUINGILIANA KIUTENDAJI
Dk Kigwangalla anasema mawaziri kufanya shughuli za kijamii kama ukusanyaji wa fedha za miradi ya maendeleo si jambo baya.
“Kwa hiyo waziri mmoja anapokwenda kutekeleza majukumu kwenye sekta
ya waziri mwingine, siyo mbaya isipokuwa waziri anayefanya hivyo
asiwe na nia zinazojificha na pia asitumie vibaya nafasi hiyo kumkashifu
mwenzake anayesimamia sekta husika,” anasema.
HALI SIASA NDANI YA CCM
Anasema, Chama Cha Mapinduzi kipo juu kiutendaji na namna
kinavyokubalika kwa umma kwa sababu nyingi mbalimbali mojawapo ikiwa ni
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya 2010.
“Ni chama kipo madhubuti, hakiyumbiyumbi, migogoro yake kinaitatua
kwa utaratibu, wanachama wanaelewana, hata kama wanatofautiana
mitazamo,” anasema.
Anasema, wabunge wa CCM na viongozi wa chama hicho wanafanya ziara
kwa wananchi, wakielezea mafanikio katika utekelezaji wa ilani hiyo.
“Ninaamini kwa kuwa wananchi wameona mafanikio hayo, kukubalika kwa chama kumezi kuongezeka,” anasema.
SHINIKIZO KWA MAWAZIRI KUJIUZULU
Dk Kigwangalla anasema uwajibikaji wa viongozi wa CCM na kwa
waliopo serikalini (mawaziri) si jambo la leo, bali la siku nyingi,
akitoa mfano wa kujiuzulu kwa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
Mwinyi aliwajibika kwa makosa yaliyotokea mkoani Shinyinga, yakifanywa na watu walio chini yake.
“Sioni kama ni jambo la ajabu kwa viongozi hawa kuwajibishwa ama
kuwajibika kwa makosa yaliyofanywa na watendaji ama walinzi wengine wa
amani ambao walitumwa kwenda kutekeleza operesheni tokomeza ujangili,”
anasema.
“Kwa hali yoyote ile, kiongoza mwadilifu na mzalendo, huwezi
kukubali yale yaliyofanywa kwa raia wenzatu, yale mateso waliyopewa
huiwezi kuyakubali, utayakataa na hata kama hukuyafanya, lakini
yalifanywa chini yako na kama wewe ni mzalendo, ni mwajibikaji wa
ukweli, utawajibika tu,” anasema.
Anaongeza, “ukiziona zile picha, ukisikiliza hadithi za mambo
yaliyofanyika, huwezi kukubali, kwa hiyo hilo mimi sioni kama
linatupasua na sioni kama ilibidi Waziri Mkuu kujiuzulu, wakati walio
chini yake walikubali na kuamua kuwajibika.”
Dk Kigwangalla anasema Waziri Mkuu amebakisha miaka miwili katika
utawala wa awamu ya nne, kuna mambo anayoyatekeleza hivyo kumbadilisha
kungeiyumbisha serikali.
CHANGAMOTO NDANI YA CCM
Anasema, changamoto ni kubwa kwa sababu taifa bado ni changa.
Matatizo na kero zilizopo ni nyingi na haiwezekani kuzimaliza kabla ya
2015.
“Tumejitahidi kufanya kazi kwa kadri ya uwezo wetu, tumeonyesha
matumaini kwamba matatizo yanayowakabili wananchi yanatatulika,”
anasema.
Anatoa mfano kuwa, barabara Nzega-Tabora, ilikuwa ya vumbi, ambapo ilani ilieleza itajengwa kwa kiwango cha lami.
“Tumechelewa kuikamilika, lakini lami imeanza kumwagwa, madaraja
yote yamejengwa. Hata kama haijakamilika, kwa mwananchi mwenye akili
zake timamu na ambaye anaangalia mambo kwa uhalisia, atakubaliana kazi
inafanyika na itaisha, atapata matumaini,” anasema.
USHIRIKI WA VIJANA KATIKA SIASA NDANI YA CCM
Dk Kigwangalla anasema kushabikia ama kuwa mwanachama wa chama
chochote ni haki za msingi, zinazolindwa na Katiba katika uhuru wa
kuchagua.
“Hivyo si lazima vijana wote wawe CCM. Lakini sisi tulioshika dola
tuna ulazima wa kulinda demokrasia na watu washirkiki michato kwa uhuru
amani na uchaguzi unaolindwa na Katiba,” anasema.
Hata hivyo, anasema kupata ushawishi kwa vijana, lazima CCM idumu
katika misingi ya uadilifu, uzalendo na kujenga mikakati na sera za
kuwakomboa vijana.
KUPINGANA NA VIONGOZI WA CHAMA NA SERIKALI
Dk Kigwangala, anasema kuonekana kwake kupingana na baadhi ya
viongozi wa CCM na serikali kunatokana na tofauti za uelewa wa misingi
ya chama hicho.
“Chama hiki kimejengwa na misingi, kina mambo kinayoyasimamia
mojawapo ni uhuru wa kuongea, kukosoa, kujikosoa mwenyewe na kukosoana,”
anasema.
Anasema, “nguvu ya kukosoa na kuwapinga miongoni mwa viongozi
wenzangu, ninaitoa kwenye misingi ya chama, kwa sababu mimi nimeisoma
katiba, sikuingia CCM uzeeni.”
“Nimezaliwa na wazazi wa CCM, babu zangu walikuwa waasisi wa Tanu,
walikuwa viongozi na nimepitia chipukizi, nimecheza halaiki, nimekuwa
kiongozi ngazi ya wilaya na UVCCM,” anasema.
“Unajua kuna viongozi waliopitia CCM na waliotokana na CCM. Mimi ninatokana na CCM, wengine wamepitia CCM kuchukua uongozi.”
“Sasa kundi la viongozi waliopitia CCM kwa maana kwamba hawajui
misingi ya CCM, hawajui nguzo za uimara wa CCM wanapata taabu
wanapokutana na mtu anayesenma ukweli kama mimi.”
“Sasa mimi ninayekosoa utanichukia bure, sawa sawa na mtu mwenye
chunusi kukichukia kioo kwa kuzionyesha chunusi hizo. Anapaswa kusafisha
chunusi zake, aponyeshe ugonjwa na ngozi yake ikiwa laini, kioo
hakitamdanganya, kitamuonyesha ukweli.”
KATIBA MPYA
Anasema, kuna mambo mengi yanayopaswa kufikiriwa katika Katiba Mpya, mojawapo ni serikali tatu.
“Lakini kama kuna kitu ambacho Watanzania tunatakiwa tuwe makini,
kuhakikisha kinabadilika ni kurekebisha mfumo wa uwajibikaji,” anasema.
“Kwamba tunawawajibisha vipi watendaji na wanasiasa wetu. Hayo ni
mambo ya msingi yanapaswa kuangaliwa sana katika Katiba Mpya.”
“Kwa mfano mambo ya mikataba ya ardhi, madini, rasilimali nyingine
maliasili, vitalu, misitu ingepaswa kwa kiasi kikubwa sana kuwa ni
sehemu ya kupata baraka za Bunge kama ilivyo leo, lakini kasheria
kanakolinyang’anya Bunge mamlaka hayo, kaondolewe,” anasema.
“Jambo lingine ni nafasi ya Bunge juu ya uteuzi wa viongozi wa mashirika ya umma kama wizara za serikali, mahakama.”
“Mifumo ya uwajibikaji wa wakuu wa mikoa na wilaya kazi zao ni kama
hazieleweki, ikitokea fursa ya kuiendesha mikoa yetu, inapaswa viongozi
hao kuwa juu ya Wakurugenzi Watendaji” anasema. Anasema, baadhi ya
Wakurugenzi hao wamekuwa wabovu, wanafanya kazi chini ya viwango na
wabadhirifu.
SOURCE:
NIPASHE JUMAPILI
By Mashaka Mgeta
Post a Comment