Home » , » UPDATES: Uchaguzi wa Papa Vatican

UPDATES: Uchaguzi wa Papa Vatican

Written By peterdafi.blogspot.com on Wednesday, March 13, 2013 | 2:54 AM

Makardinali wako tayari kwa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro



Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumanne
tarehe 12 Machi 2013, saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya,
anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, itakayohudhuriwa na
Makardinali pamoja na Familia ya Mungu kwa ajili ya kuombea
uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mkutano wa Makardinali umeamua kwamba, Kikao cha uchaguzi wa Papa Mpya kitaanza
rasmi Jumanne, tarehe 12 Machi 2013. Majira ya saa 10:30 Jioni kwa saa za Ulaya,
Makardinali wataingia kwenye Kikanisa cha Paulo, tayari kuingia kwenye Kikanisa cha
Sistina, wakiongozwa na nyimbo za kuomba mapaji ya Roho Roho Mtakatifu
wanapoanza kutekeleza dhamana hii nyeti kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa la
Kristo.

Kikao hiki kitaanza kwa Makardinali kula kiapo cha siri kadiri ya sheria na kanuni za
Kanisa. Conclave inapoanza, lango linafungwa na hapo waamini wanaendelea
kuwasindikiza Makardinali kwa njia ya sala, wakisubiri kuona moshi mweupe alama
kwamba, Kanisa limempata Papa Mpya!

Wakati huo huo, Maafisa na wote watakaohusika na shughuli za Conclave, tarehe 11
Machi 2013, majira ya jioni wanakula kiapo cha kutunza siri za uchaguzi wa Papa Mpya
kama ilivyoamriwa na sheria pamoja na kanuni za Kanisa. Ibada ya kula kiapo itafanyika
kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Paulo.

Padre Federico Lombardi akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa juma,
amefafanua kwamba, Makardinali wataanza kuingia kwenye vyumba walivyopangiwa
kwenye Hosteli ya Sanctae Marthae iliyoko ndani ya mji wa Vatican, tarehe 12 Machi
2013, kuanzia saa 1:00 na kuendelea, ili kuwapatia nafasi ya kujiandaa kwa ajili ya
kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Khalifa wa
Mtakatifu Petro, hapo saa 4:00 asubuhi.

Mkutano wa Makardinali unaendelea hata Jumatatu, ili kutoa nafasi kwa Makardinali
ambao walikuwa bado hawajashirikisha mawazo yao kuzungumza kabla ya kuanza
rasmi mchakato wa kumchagua Papa Mpya. Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV
kitarusha picha maalum katika matukio haya maalum wakati wahudumu wa Conclave
wa kula kiapo kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya.

Hatua za mwisho mwisho kabla ya Papa Mpya kutokeza hadharani!

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican
anabainisha kwamba, uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro
unakamilika kwa Kardinali kupata theluji mbili ya kura zote
halali zilizopigwa. Baada ya hapo, Dekano wa Makardinali
ambaye wakati wa uchaguzi ni kardinali Giovanni Battista Re,
atamuuliza Kardinali aliyechaguliwa kama anakubali kisheria kwamba, amechaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.


Baada ya hapo, ataulizwa jina ambalo atalitumia katika utume wake kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro. Wakati wote huu, Mshehereheshaji mkuu wa Papa ndiye atakayekuwa
anachukua rasmi taarifa zinazotolewa na Papa Mteule akisaidiwa na Washereheshaji
wengine wawili wanaokuwepo mahali hapo kama Mashahidi. Seehemu hii ya mchakato
ikikamilika, hapo karatasi zilizotumika kwa ajili ya kupigia kura zinachomwa na hapo
moshi mweupe unatoka kuashiria kwamba Kanisa limempata Papa Mpya.

Papa Mpya ataelekea kwenye "Chumba cha machozi" neno ambalo pengine linaonesha
ile hali ya ndani anayokuwa nayo Kardinali baada ya kuambiwa kwamba, amechaguliwa
kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anaporudi kwenye Kikanisa
cha Sistina, Injili inayozungumzia Ukulu wa Mtakatifu Petro inasomwa, Makardinali
wanasali kwa kitambo kidogo na hapo Makardinali moja baada ya mwingine wanaanza
kwenda kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati wote huu, Makardinali na Papa wanaendelea kumshukuru Mungu kwa kuimba utenzi wa shukrani,
Te Deum.

Padre Lombardi anasema, Papa Mpya kabla ya kwenda kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la
Mtakatifu Petro kutoa baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu kwa ujumla, "Urbi et
Orbe" atapitia kwanza kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Paulo kusali kwa kitambi kifupi na
baadaye atawasalimia na kuwapatia baraka zake za kitume waamini, mahujaji na wote
watakaokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Papa
mpya ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kusimikwa kwake, siku yoyote inayoonekana inafaa zaidi!
Mabadiliko katika Liturjia za Kipapa



Monsinyo Guido Marini mshereheshaji wa Liturujia za Kipapa anasema, Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, tarehe 18 Februari 2013 aliruhusu
kufanya marekebisho katika Ibada ya mwanzo wa utume wa Khalifa wa
Mtakatifu Petro, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo kuu la Roma anayepewa
dhamana ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu

Papa mpya anawajibika kutembelea Makanisa makuu yaliyoko mjini Roma, yaani: Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu pamoja na Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa
Laterano, Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma.
Kabla ya mageuzi yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Papa
Mpya baada ya kuchaguliwa tu, siku ya pili alikuwa analazimika kwenda kutembelea
Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Kwa sasa Baba Mtakatifu anaweza kutembelea Kanisa
hilo pale atakapoona inafaa kadiri ya taratibu zake. Tukio hili litafanyika nje ya Ibada ya Misa Takatifu.

Baba Mtakatifu Mpya atakapoanza utume wake rasmi, ataadhimisha Ibada ya Misa
Takatifu itakayohudhuriwa na Makardinali wote watakaokuwepo na baadaye watakula
kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Itakumbukwa kwamba, mara tu baada ya
uchaguzi kwenye Kikanisa cha Sistina, Makardinali wanakula kiapo cha utii kwa Khalifa
Mpya wa Mtakatifu Petro. Tendo hili linachukua mwono wa hadhara katika Ibada pamoja na kukazia ile dhana ya Kanisa moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume.

Haitakuwa kwa mara ya kwanza kwa Ibada hii kufanyika kwani Mwenyeheri Yohane
Paulo wa pili aliianzisha na imeendelea kuwa ni kumbu kumbu ya pekee katika maisha
na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mabadiliko mengine yaliyofanywa katika Ibada
za Kipapa ni ile ya kuwatangaza wenyeheri kuwa watakatifu, Mkesha wa Pasaka pamoja
na Ibada ya kuwavisha Palio takatifu Maaskofu wakuu.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger