Home » , » Nani atazima moto wa Lowassa CCM

Nani atazima moto wa Lowassa CCM

Written By peterdafi.blogspot.com on Wednesday, February 5, 2014 | 10:08 AM


Nguvu ya makundi ya watu wanaotajwa kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaendelea kukitikisa chama hicho huku makada wake wakitoa angalizo wakiutaka uongozi wa juu wa kuchukua hatua haraka za kinidhamu kwa wahusika.
Wiki iliyopita wanachama wa chama hicho wanaodaiwa kutoka katika kambi tofauti zinazoisaka nafasi ya urais waliibuka na kutoa kauli zinazoonekana wazi kupigana vijembe, kila upande ukiuponda mwingine kuwa unavunja kanuni na katiba ya chama hicho.
Malumbano hayo ya makada wa CCM yanayoonekana dhahiri kuchagizwa na makundi pamoja na wafuasi wa vigogo wanaousaka urais kupitia chama hicho.
Ingawa makundi yanayosaka urais kupitia chama hicho ni mengi, ni kundi moja tu linalomuunga mkono aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa ndilo linaloonekana dhahiri kupigiwa kelele kwa kutajwa kwa majina bila kificho, hasa baada ya kauli yake kuwa ameanza safari, aliyoitoa mbele ya wageni wakati wa kuadhimisha mwaka mpya 2014.
Kutokana na kauli hiyo na mambo mengine, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa UV-CCM, Paul Makonda aliibuka na kumshambulia Lowassa, suala ambalo limeyaibua makundi mengine, baadhi yakiunga mkono kauli ya Makonda na mengine yakiibeza na kumshushia tuhuma za kuvunja kanuni za chama.
Mmoja kati ya waliojitokeza ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela ambaye ameonyesha waziwazi kutofautiana na mipango na mikakati ya Lowassa.
Malecela anamuunga mkono Makonda, kwa kauli yake, ikiwamo kwamba Lowassa anafadhili mikakati ya kupingana na juhudi za sekretarieti ya CCM chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Wakati Makonda na Mzee Malecela wakitoa tuhuma hizo, makundi mbalimbali ya Jumuiya ya Vijana UVCCM nao wameibuka na kumshutumu Makonda kuwa aliyoyasema ni maoni yake na siyo msimamo wa Jumuiya hiyo.
Kauli hiyo ya Makonda imeibua malumbano baina ya viongozi wa jumuiya hiyo, wengi wakimshutumu kwa "kutumiwa kumchafua Lowassa" na kwamba kauli aliyoitoa ni ya kwake na idara yake, wala isihusishwe na Umoja wa Vijana wa CCM.
Baadhi ya waliojibu ni pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia kundi la vijana, Jonas Nkya na Ramadhani Kimwaga, pamoja na Mjumbe wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo Mkoa wa Mbeya, Adam Mwakalinga.
Vijana hao kwa nyakati tofauti wanasema wamehuzunishwa na matamshi ya Makonda akimshutumu Lowassa na kutamka kuwa umoja huo hautaki kuingizwa katika masuala binafsi ambayo yanaweza kukigawa chama na jumuiya zake.
Mwakalinga anasema Makonda anapaswa kufanya kazi ya idara yake ya watoto badala ya kukurupuka na kutaka kuwaaminisha Watanzania kuwa Edward Lowassa si kiongozi mzuri huku akijua wananchi wenyewe na hata wapinzani wanaona uthubutu wake katika maendeleo hasa kwa vijana.
Kauli ya Sadifa
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis anasema kutangaza nia ya kugombea nafasi yoyote ndani ya chama si kosa mradi tu mhusika ataridhika kuwa na nia, sifa na uwezo wa kile anachokisema.
Anasema ingawa UVCCM haijakaa kujadili watu hao, lakini haoni kosa lolote kwa mwanaCCM kujitokeza na kutangaza nia yake hadharani.
"Nikuulize mwandishi, kutangaza nia ni kosa? Kama mtu ameamua kueleza nia yake anakuwa amevunja sheria gani...sioni kosa lolote endapo mtu ameeleza nia yake baada ya kujiona anazo sifa, uwezo hiyo ni haki kikatiba," alisema
Hata hivyo, Sadifa anasema kosa analoliona na ambalo ni kinyume na kanuni za chama ni kwa mtu kujipitisha na kuanza kusaka kuungwa mkono ingawa alikiri kuwa kwa yeye kama mwenyekiti hakuna aliyejitokeza kuomba amuunge mkono.
Anaongeza kusema kuwa kauli iliyotolewa na Makonda si ya Jumuiya kwa kuwa UVCCM haimuungi mkono mgombea yeyote.
"Msemaji wa UVCCM ni mmoja kitaifa na ndiyo mimi, hakuna msemaji mwingine...yaliyosemwa na Makonda ni yake mwenyewe na siyo msimamo wa jumuiya," anasema.
Anaongeza kuwa ingawa Makonda anayo haki ya Kikatiba kutoa maoni yake lakini siyo sahihi wala busara kwa mwanachama kumsema mwanachama mwingine hadharani, badala yake mambo hayo yangepaswa kujadiliwa kwenye vikao vya ndani vya chama.
Wito kwa wanaCCM
Sadifa anatoa wito kwa makundi yote yanayoibuka na yaliyopo ndani ya chama hicho kutulia kwa kile alichosema muda wa kampeni haujafika na kwamba hali hiyo ikiendelea itasababisha chama kushindwa kumpata mgombea safi maana wote watakuwa wameshachafuka.
"Ushauri wangu ni kwa wanaCCM wote kuwa watulivu kwa faida ya chama...kuchafuana au kuharibiana ni kukiharibia chama kwani wakati ukifika tutashindwa kumpata mgombea safi," anasema Sadifa.
Kauli ya Msekwa
Wakati malumbano hayo yakiibuka, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa anawaonya wanachama wa chama hicho wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao kuzingatia kanuni za chama hicho, vinginevyo watahukumiwa kwa mujibu wa kanuni zenyewe.
Msekwa anasema kutangaza nia kabla ya wakati ni kukiuka kanuni za chama ambazo zinaeleza wazi kuwa wagombea wa nafasi mbalimbali watajitangaza baada ya chama kutoa ratiba yake.
Anasema CCM inaongozwa kwa mujibu wa kanuni na katiba yake na kwamba katika jambo hili linaloibuka sasa kanuni ndiyo zinayohusika ambazo zinaeleza wazi mgombea afanye nini na kwa wakati gani.
"Mimi mwenyewe nilishiriki kuandika hizi kanuni, utakapofika wakati, chama kitatoa ratiba yake na kila mwenye nia atakuwa na uhuru wa kueleza nia yake, lakini kutangaza kugombea sasa kabla ya wakati ni kukiuka kanuni za chama na ni kosa kubwa," anasema Msekwa.
Msekwa anatoa angalizo kwa wale wanaodhani kuwa kwa kuvunja kanuni wanakivuruga chama, badala yake wahusika wanafanya makosa yatakayowaathiri wenyewe.
Hii si mara ya kwanza kwa Msekwa kukemea makundi ndani ya chama hicho, akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, wakati akiwahoji watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho, alipata kusema makundi ya wanaowania urais, yanakivuruga chama na kuwa hakitawavumilia wanaochochea migogoro hiyo kwa masilahi yao binafsi. Chanzo: mwananchi
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger