HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE YA KUADHIMISHA SIKU YA
SHERIA NCHINI, TAREHE 04 FEBRUARI, 2015
DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania;
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania;
Mheshimiwa Asha-Rose Migiro, Waziri wa Katiba na Sheria;
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Shabani Ali Lila, Jaji Kiongozi;
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania;
Mheshimiwa George Masaju, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ;
Waheshimiwa Majaji Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani wastaafu;
Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Wasajili, Wakurugenzi na Watendaji wa Mahakama;
Mahakimu na Mawakili;
Mtendaji Mkuu wa Mahakama;
Watumishi wa Mahakama;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kunialika kwa mara nyingine tena
kushirikiana nanyi katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Tanzania. Hii ni mara
yangu ya nane na ya mwisho kuhudhuria sherehe hizi nikiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Sherehe za mwakani zitahudhuriwa na Rais mpya.
Natumai mtaendelea kumualika.
Napenda kuwashukuru wale wote tulioshirikiana nao katika utekelezaji wa jukumu
zito la kuimarisha mhimili wa Mahakama katika kipindi changu cha uongozi.
Napenda kukutambua, wewe mwenyewe Mheshimiwa Mohamed Chande Othman
na Majaji Wakuu waliokutangulia, Mheshimiwa Barnabas Samata niliyemkuta na
Mheshimiwa Augustino Ramadhani aliyemfuatia. Nawashukuru kwa ushirikiano
wenu, umakini, weledi na umadhubuti wa hali ya juu kwa kuwaongoza wenzenu
vizuri katika kutoa haki nchini. Nyote mlikuwa kielelezo kizuri cha utoaji haki hapa
nchini na kioo cha uongozi bora wa Mahakama yetu. Pamoja nanyi nawashukuru
Majaji wote wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu, Wasajili, Mahakimu
Wakazi, Mahakamu wa Mahakama ya Mwanzo ambao wote mmejitoa kusimamia
utoaji wa haki katika nchi yetu. Vile vile, namtambua Mtendaji Mkuu wa
Mahakama na Watendaji wa ngazi zote pamoja na watumishi wote wa Mahakama
kwa kazi yao nzuri waifanyayo.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu yaani, “Fursa ya Kupata Haki: Wajibu
wa Serikali, Mahakama na Wadau” ni muafaka kabisa kwa wakati uliopo. Inatoa
fursa kwa mihimili yetu miwili ya dola na wadau wengine kupima jinsi
tunavyotimiza wajibu wetu. Naomba tutumie fursa hii tuangalie yale tuliyofanya
katika kipindi cha miaka tisa (9) ya uongozi wangu kuhusu kuimarisha utoaji wa
fursa ya kupata haki nchini.
Kuboresha utoaji wa haki na utawala wa sheria nchini ilikuwa miongoni mwa
mambo tuliyoyapa umuhimu wa juu katika majukumu ya Serikali yetu. Kwa ajili
hiyo tumejitahidi kutambua mahitaji na changamoto zilizokuwa zinaikabili
Mahakama nchini na kujaribu kutafuta majawabu. Tumechukua hatua na kufanya
mambo mbalimbali kwa madhumuni ya kuiwezesha Mahakama kutekeleza wajibu
wake wa kutoa haki.
Fursa ya Kupata Haki
Mheshimiwa Jaji Mkuu,
Kama ulivyosema, wewe mwenyewe fursa ya kupata haki imegawanyika katika
sehemu mbili. Kwanza, ni fursa ya kuifikia Mahakama, na pili, ni fursa ya
kunufaika na huduma za Mahakama yaani kupata haki. Dhana hii inazilazimu
Serikali na Mahakama kufanya kazi kwa pamoja, kwani mhimili mmoja pekee
hauwezi kufanikisha haya yote mawili. Kimsingi, Serikali inao wajibu wa kuweka
mazingira mazuri kwa Mahakama kuweza kutimiza wajibu wake huo wa kutoa
haki kwa wakati.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Ninapoiangalia Mahakama ya leo ninafarijika kuona kwamba hatua zilizochukuliwa
na Mahakama yenyewe na nyingine zilizochukuliwa kwa kushirikiana na Serikali
zimesaidia kuleta mabadiliko kwenye mifumo na kuboresha utoaji wa haki.
Changamoto za kimfumo zilizokuwapo ziliathiri ufanisi katika utoaji haki nchini
hususan zilisababisha ucheleweshaji wa mashauri na hukumu.
Hali hii imefanya utatuzi wa migogoro ya mikataba, biashara, ardhi, mahusiano
kazini kuchelewa sana (labor matters). Kwa ujumla, jitihada zetu za kukuza
uchumi zilipambana na vikwazo vya mifumo yetu ya sheria. Hali kadhalika, kwa
upande wa mifumo ya haki jinai, taratibu za kuendesha mashauri hazikuakisi
mahitaji ya kutoa haki kwa kuadhibu wakosaji kwa wakati na kutoa fidia na ahueni
nyingine inayofaa kwa wahanga wa uhalifu.
Mambo mengi yamefanyika kuboresha Mahakama. Tumetunga Sheria namba 4 ya
mwaka 2011 ya uendeshaji Mahakama ambayo pamoja na mambo mengine
ilianzisha Mfuko wa Mahakama na kuwezesha Mahakama kuwa na bajeti
inayotabirika na ya uhakika. Fedha za Mfuko huu zimekuwa zikiongezeka kutoka
bilioni 57.8 mwaka 2012/2013 hadi bilioni 89.6 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko
la asilimia 54.8. Katika mfumo huu mpya tumeanza sasa kutenga bajeti ya
maendeleo inayowezesha uwekezaji katika upatikanaji wa miundombinu ya utoaji
haki. Nimesikia mwaka huu bajeti ya maendeleo haijaingia, naomba niwahakikishie
kuwa mtaipata. Jana nilizungumza na Waziri wa Fedha aliyenihakikishia kuwa
katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha wataanza kutoa fedha.
Jambo lingine muhimu tulilofanya lilikuwa ni kuongeza rasilimali watu.
Tumepunguza uhaba mkubwa uliokuwepo na kuwezesha Mahakama kuboresha
kazi yake ya kutoa haki. Hivi sasa kuna Majaji wa Rufani 16 kutoka 9
waliokuwepo mwaka 2005 na kuna Majaji wa Mahakama Kuu 81 kutoka Majaji 35
waliokuwapo 2005. Ninafurahi kuwa kati ya Majaji wote wa Mahakama ya Rufaa
na Mahakama Kuu waliopo, Majaji 38 sawa na asilimia 39.2 ni wanawake. Haya ni
mageuzi makubwa. Natambua kuwa mahitaji halisi ni kuwa na Majaji 120.
Napenda kukuhakikishia Mheshimiwa Jaji Mkuu kuwa mtakapokuwa tayari
nileteeni mapendekezo yenu nifanye uteuzi. Kwa upande wa Mahakimu Wakazi,
hadi mwaka huu idadi yao ilifikia 677 nchi nzima ukilinganisha na Mahakimu
Wakazi 151 mwaka 2005. Mwaka wa jana pekee tulitoa kibali cha kuajiri
Mahakimu wapya 300.
Katika kipindi hiki pia tulifanya mambo mawili mengine muhimu kwa utekelezaji
mzuri wa majukumu ya Mahakama. Kwanza ni lile la kukamilisha mchakato wa
kutenganisha shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka. Imesaidia
kupunguza ucheleweshaji wa mashauri na kuimarisha utoaji wa haki.
Jambo la pili ni kuanzishwa kwa nafasi ya Watendaji wa Mahakama iliyo
waondolea Majaji majukumu ya utawala na fedha na kuwaaacha washughulike na
utoaji wa haki. Jambo hili limeboresha na kuimarisha utendaji na uendeshaji wa
shughuli katika Mahakama kwa namna ambayo haijawahi kuwepo huko nyuma.
Huduma ya Msaada wa Kisheria
Mheshimiwa Jaji Mkuu,
Nakubaliana nawe kuwa kukosekana kwa msaada wa kisheria kwa wale wasio na
uwezo wa kulipia huduma ya uwakili ni kikwazo kwa watu hao kupata fursa ya
kupata haki. Pia inakwaza utoaji wa haki. Nimefurahishwa na pendekezo lako la
kuiomba Serikali kuona uwezekano wa kugharamia huduma za uwakili kwa
watuhumiwa wasio na uwezo kifedha nje ya watuhumiwa wa makosa ya mauaji.
Umeomba sasa tuangalie na wale wenye makosa yenye adhabu kubwa na vifungo
virefu. Nakubaliana nawe kuwa wakati sasa umefika wa kuyaangalia mambo hayo
kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyotokea nchini ikiwemo kuongezeka kwa
aina ya makosa, adhabu na kuwepo kwa Wanasheria wa kutosha wa kuweza
kutoa huduma hiyo ni jambo linalowezekana. Sisi katika Serikali tutalifanyia kazi
pendekezo hilo na tutawashirikisha mtupe maoni yenu ya namna bora ya
kutekeleza wazo hili. Naamini, tukifanya hivyo, tutakuwa tumepanua fursa kwa
watu wengi kupata haki ya kisheria.
Wajibu wa Mahakama
Mheshimiwa Jaji Mkuu,
Kama nilivyosema awali, fursa ya kupata haki inategemea pia jinsi Mahakama
inavyotelekeza ipasavyo wajibu wake. Nafurahishwa sana na hatua ambazo Jaji
Mkuu umechukua ambazo zimewezesha kuboresha fursa ya kupata haki. Taarifa
uliyoitoa hapa leo imeonesha wazi mafanikio yaliyopatikana. Kufuatia uamuzi
wenu wa kujiwekea ukomo wa muda wa kuendesha kesi na idadi ya kesi kwa kila
Jaji na Hakimu, mmeweza kupunguza mashauri ya siku nyingi kwa asilimia 50
kutoka mashauri 6,887 mwaka 2012 hadi 3,632 katika Mahakama Kuu mwaka
2014. Aidha, mmeweza kumaliza mashauri 52 kati ya 59 yanayohusu miradi
mikubwa ya serikali iliyoko katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Natoa rai kwa wadau wengine wa sheria yaani waendesha mashtaka na vyombo
vya upelelezi kwa upande wa mashauri ya jinai pamoja na Mawakili wa
kujitegemea kuunga mkono juhudi zenu hizi. Bila shaka Mahakama itaendelea
kuonyesha njia kwa kusimamia mwenendo wa mashauri ya jinai na madai pasipo
kuchelewesha. Ni matumaini yangu kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka na vyombo
vya upelelezi havitakuwa chanzo cha kuchelewesha mashauri pasipo sababu za
msingi.
Kusogeza Huduma ya Mahakama karibu zaidi na Wananchi
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Natoa pongezi nyingi kwamba kwa sababu ya mambo mbalimbali mazuri
yaliyofanyika ambayo yamesogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi.
Sehemu kubwa ya migogoro inayowagusa moja kwa moja wananchi
imeshughulikiwa. Miongoni mwa hiyo ni ile ya ardhi ambapo Mabaraza ya Ardhi
yameundwa katika Kata zote nchini chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi. Jambo hili limepunguza sana mzigo wa mashauri katika
Mahakama zetu na kusaidia kuleta usuluhishi katika jamii zetu. Inawezekana
utendaji wa vyombo hivi una upungufu mbalimbali kinyume cha matarajio ya
wananchi. Dawa yake siyo kuvitelekeza bali kuyatambua matatizo yaliyopo na
kuyapatia ufumbuzi.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Halmashauri za
Wilaya waendelee kusimamia kwa karibu vyombo hivi muhimu kwa kusogeza
huduma ya upatanishi na kushughulikia migogoro midogo ya ardhi. Kuna
malalamiko ya kutokuwepo kwa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya katika Wilaya nyingi
nchini. Kwa sababu hiyo watu wamekuwa wanapata usumbufu katika kutafuta
haki baada ya kutokuridhishwa na uamuzi wa Mabaraza ya Kata. Wizara
iharakishe kuunda Mabaraza hayo na Halmashauri zisaidie upatikanaji wa majengo
ya Mabaraza hayo.
Uhusiano wa Mabaraza ya Ardhi na Mahakama Kuu
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Naambiwa kuwa yapo malalamiko ya kukosekana mtiririko mzuri wa majalada
kwenda Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi. Nia njema ya kuanzisha Mabaraza ya
Ardhi imezaa adha. Kilio kilichopo ni kwamba Mabaraza hayo yamekuwa hayataki
kutii amri ya Mahakama Kuu ya kupeleka kumbukumbu pindi kunapokuwa na rufaa
dhidi ya maamuzi yake ni jambo ambalo sio tu halikutarajiwa bali halikubaliki.
Linatia dosari katika utoaji wa haki ya ardhi. Wakati huo huo, Wizara ya Ardhi
iwachukulie hatua zipasazo watendaji wa Mabaraza ya Ardhi wanaochelewesha
kumbukumbu.
Ni matumaini yangu kuwa wadau wanaohusika yaani Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Katiba na Sheria na Mahakama mtakaa pamoja
mapema iwezekanavyo kulitafutia ufumbuzi tatizo hili. Kama itahitaji kupitia upya
sheria na taratibu ifanyike hivyo ili kuondoa kikwazo hiki na kuondoa malalamiko
yanayoendelea kwa muda mrefu sasa kuhusu jambo hili. Ipo rai kwamba Sheria
iwawajibishe watendaji wa Mabaraza ya Ardhi kwa Mahakama Kuu moja kwa
moja. Busara na hekima ya kufanya hivyo itafakariwe kwa makini. Ni matarajio
yangu kwamba hatua hizi zitachukuliwa mapema na pale kwenye mkwamo
tuambiane tuone namna ya kusaidia kukwamua.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Nimefarijika sana kusikia kwamba mkakati uliopo sasa ni kuongeza weledi kwenye
Mahakama za Mwanzo kwa kuendelea kuajiri wahitimu wa Shahada ya Sheria
kwenye Mahakama hizo. Hili ni jambo zuri ambalo litawawezesha Mawakili
kusimamia na kuendesha kesi kwenye Mahakama za Mwanzo. Madhali sasa,
hatuna uhaba wa Wanasheria na Mawakili, hili linawezekana. Uamuzi wetu wa
kupanua huduma ya Mahakama Kuu kila Mkoa ni mwendelezo wa dhamira yetu ya
kuwafanya wananchi waweze kuifikia huduma hiyo karibu na wanapoishi. Bado
tunayo dhamira ya kukamilisha ujenzi wa Mahakama Kuu kila mkoa ifikapo mwaka
2016 kama tulivyoagiza. Utekelezaji wa dhamira hii unakwenda sambamba na
uteuzi wa Majaji wengi wa Mahakama Kuu kama nilivyoeleza awali.
Mapendekezo yako, Mheshimiwa Jaji Mkuu, ya kupitia upya taratibu zilizopo ili
kufanya utatuzi wa migogoro na utoji haki uwe rahisi na unaoeleweka kwa
wananchi ni mzuri. Sehemu kubwa ya mashauri ya madai yanahusu usuluhishi.
Kinachotakiwa ni kwa wanaosuluhishwa kuelewa na kuridhika na utaratibu
uliotumika kusuluhisha migogoro yao. Nakuomba, Mheshimiwa Jaji Mkuu na
wenzako myafanyie kazi mapendekezo hayo ili nchi yetu iwe na mfumo rahisi
unaoeleweka wa kutatua migogoro kwa haki, wepesi na haraka. Tukiweza kufikia
lengo hili, wananchi wataiona Mahakama ni chombo cha kutatua migogoro na siyo
mahali pageni pasipofaa kufika hata kama mtu hana budi kufanya hivyo. Hii
itaondoa kishawishi kwa wananchi kutafuta njia nyingine zisizofaa kupata haki
zao. Tusikubali tufike huko.
Hitimisho
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kurudia kukushukuru kwa kunialika kuja
kujumuika nanyi siku hii adhimu. Katika kipindi hiki tumefanya mambo mengi
yaliyoleta mabadiliko madogo na makubwa katika mifumo ya utoaji wa haki nchini
na kuongeza ufanisi. Nawashukuru wale wote tulioshirikiana katika kuleta
mabadiliko haya. Busara za Majaji Wakuu watatu walioiongoza Mahakama, Majaji
wa Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Wasajili, Mahakimu na watumishi wengine
wa Mahakama ni hazina kubwa na ya kujivunia. Ushirikiano wa wadau mbalimbali
umetusaidia kufikia hapa tulipo sasa. Naamini kama watu wataendelea kuitumikia
nchi yetu na watu wake kwa moyo wa uzalendo na kujituma tutapiga hatua kubwa
mbele.
Baada ya kusema hayo yote naomba sasa niwatakie siku njema ya Sheria nchini.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Post a Comment