Home » , » William Ngeleja Akili kuomba na Kupokea 40.4 M toka kwa Rugemalira

William Ngeleja Akili kuomba na Kupokea 40.4 M toka kwa Rugemalira

Written By peterdafi.blogspot.com on Tuesday, March 3, 2015 | 10:10 PM

Mbunge wa Sengerema,  William Ngeleja amekiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwamba, aliomba na kupokea Sh milioni 40.4 kutoka kwa James Rugemalira, kwa kujitetea alifanya hivyo kama ilivyo kawaida pia kwa wabunge wengine.

Ngeleja  alidai mbele ya baraza hilo kwamba, msaada huo aliopewa na Rugemalira hauna tofauti na  mingine aliyowahi kupokea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kama vile Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa na Yusuf Manji.
 
“Msaada niliopewa na Rugemalira hauna tofauti na misaada mingine wanayopewa wabunge wenzangu au misaada mingine niliyowahi kupokea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kama vile akina Mengi, Bakhresa, Yusuf Manji, mashirika ya hifadhi ya jamii kama vile NSSF, PSPF, NHC, NHIF na benki ya CRDB na NBC,” alisema.
 
Alitoa utetezi huo baada ya kusomewa mashitaka na baraza hilo,  Dar es Salaam jana, ikidaiwa Februari 12, mwaka jana, alipokea kitita hicho cha fedha kutoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, kwa ajili ya maslahi yake kiuchumi, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
 
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus alisema mlalamikiwa ni Mbunge wa Sengerema ambaye kwa mujibu wa Sheria ni kiongozi wa umma, hivyo akiwa kama mbunge alikiuka maadili hayo ya viongozi wa umma kwa kuomba fadhila ya kiuchumi kwa Rugemalira kinyume cha Sheria.
 
Akijitetea, Ngeleja alitaka kufahamu endapo shahidi na baraza hilo kwa ujumla, linafahamu kazi na wajibu mahususi wa mbunge kwa wananchi wake.
 
Alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugamalira kupitia kampuni yake ya VIP TZS Trustees na si VIP Engineering and Marketing Limited, na kusisitiza kwamba fedha hizo alizitumia kwa ajili ya maendeleo ya miradi ya jimboni kwake, ambayo haikupangiwa fedha katika bajeti ya Serikali kulingana na uhaba wa fedha uliopo.
 
“Sijawahi kuomba wala kupokea fadhila za kiuchumi kutoka kwa Rugemalira isipokuwa kama Mbunge wa Sengerema kwa nyakati tofauti kama wabunge wengine wanavyofanya, niliomba misaada ya kiuchumi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa jimbo langu na Watanzania kwa ujumla,” alisisitiza.
 
Alisema amekuwa akipokea maombi ya misaada kama mbunge,  kutoka kwa wananchi mbalimbali yanayogusa maeneo kadhaa kama vile misikiti, makanisa, kuchangia vikundi vya wajasiriamali na hata kwenye michango ya miradi ya maendeleo, jambo linalomlazimu kuomba msaada zaidi kutoka kwa wafadhili.
 
Pamoja na kutaja wafanyabiashara na mashirika yaliyowahi kumsaidia, Ngeleja aliwasilisha vielelezo vya misaada  hiyo.
 
 Pia  aliwasilisha  kielelezo cha tuhuma zilizowasilishwa bungeni na Kambi ya Upinzani na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde dhidi ya Zitto kuwa alipokea zaidi ya Sh milioni 30 kutoka Tanapa, NSSF na kampuni inayohusishwa na akaunti ya Escrow ya Power Solution Limited (PAP).
 
Kwa mujibu wa Ngeleja, pamoja na tuhuma hizo dhidi ya Zitto kuwasilishwa bungeni na vielelezo na kutaka Zitto afikishwe mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, hakuna hatua zilizochukuliwa.
 
“Ndio maana nasema hata kama ningepokea msaada huo kutoka VIP Engineering haukuwa kwa ajili ya maslahi yangu kwa sababu ni utamaduni uliojengeka kwa kampuni duniani kote kutumia sehemu ya faida zao kusaidia jamii, lakini pia nisingekuwa mbunge wa kwanza kupokea msaada wa aina hiyo,” alisema.
 
Pamoja na utetezi huo wa Ngeleja, Cyriacus alisema utetezi uliowasilishwa na kiongozi huyo, hauna mashiko kisheria.
 
“Amejitetea kwamba fedha alizopokea zimetolewa kwa ajili ya maendeleo ya jimbo lake, lakini si kweli kwa sababu nyingine alichangia Kanisa Dar es Salaam, kutokana na hili naomba apewe adhabu kali iwe fundisho.”
 
Mwenyekiti wa Baraza hilo Jaji Hamisi Msumi, alisema baraza hilo limepokea na kusikiliza pande zote mbili na litawasilisha uamuzi wake kwa mamlaka husika ambapo itajulikana endapo mbunge huyo atahitaji kujibu mashtaka yanayomkabili au la.
 
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Cyriacus, Februari 12, mwaka jana, Ngeleja alipokea Sh milioni 40.4 kutoka kampuni ya VIP Engineering

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger