Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Kama ilivyo ada imefikia siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwaka
mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015.
Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na
kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa ndugu na jamaa zetu ambao
hawakujaliwa kuiona siku ya leo tuzidi kuwaombea mapumziko mema. Nasi
tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema atujaalie umri mrefu, afya
njema na mafanikio tele kwa kila tuliombalo katika mwaka 2015 na miaka
ijayo.
Ndugu wananchi;
Hizi ni salamu zangu za mwisho za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi
yetu. Mwakani salamu kama hizi zitatolewa na Rais wetu mpya. Mimi wakati
huo nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga nikifuatilia kwenye TV na
radio hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu akitoa
salamu zake za kwanza za mwaka mpya, itakuwa siku ya furaha na faraja
kubwa kwangu.
Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko salama na
hakuna tishio lolote la kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi yetu. Uhusiano
wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani ni mzuri. Hakuna nchi iliyo adui au
tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha usalama wa Tanzania.
Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi na watendaji wa
vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa
salama.
Uhalifu Unapungua
Ndugu Wananchi;
Taarifa za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu
vimepungua ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya uhalifu
yaliyoripotiwa Polisi yalikuwa 64,088 ikilinganishwa na matukio 66,906 katika
mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi
wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na raia wema. Naomba
ushirikiano huu uendelee mwaka ujao na miaka ijayo ili tuweze kupata
mafanikio makubwa zaidi.
Ajali za Barabarani
Ndugu Wananchi;
Nimefarijika kusikia pia kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini nayo
yanaendelea kupungua. Mwaka huu kumetokea ajali 14,048 zilizosababisha vifo
vya watu 3,534 na wengine 16,166 kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali
22,383 zilizosababisha vifo 3,746 na majeruhi 19,433. Hivyo mwaka huu
kulikuwa na ajali 8,335, vifo 212 na majeruhi 3,267 pungufu kuliko mwaka jana.
Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo ingawa bado ni nyingi mno. Naomba
yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha kupata unafuu huu mwaka huu yaendelezwe
maradufu mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ugaidi
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao
wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia
mabomu na kumwagia watu tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu 112
wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wametiwa nguvuni. Tayari
watuhumiwa 87 kati yao wameshafikishwa mahakamani na waliosalia
watafikishwa wakati wo wote. Uchunguzi unaendelea ili kuwatambua wahusika
wengine ambao hawajakamatwa.
Ndugu wananchi;
Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa vyombo
vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya kutambua mtandao
wa ugaidi nchini na kuchukua hatua thabiti za kuudhibiti. Hali kadhalika
nawashukuru raia wema waliotoa taarifa zilizowezesha haya kufanyika.
Hatupaswi kubweteka wala kudhani kuwa mambo yamekwisha. Lazima
tuendelee kuchukua tahadhari muda wote kwani hatujui adui anapanga kufanya
hujuma gani, lini na wapi.
Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya biashara na
matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa 935 wakiwemo
vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19
zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine, kilo 45 za
cocaine na kilo 81,318 za bangi zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi
kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kukabiliana na dawa za kulevya nchini kwa
mafanikio yanayoendelea kupatikana. Matunda ya kazi yao tunayaona. Naomba
juhudi ziongezwe maradufu mwaka ujao na miaka ijayo. Serikali itaendelea
kuwaunga mkono.
Ndugu wananchi;
Kama nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na Kupambana
na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa
Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu. Pamoja na kupendekeza kuongeza
adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, Muswada huo pia
unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye nguvu cha kuzuia na
kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu ukipitishwa na kuwa Sheria
tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya
dawa za kulevya nchini.
Ujangili wa Wanyamapori
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka tunaomaliza leo mapambano dhidi ya ujangili na biashara
haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori yameimarishwa. Kwa ujumla
kasi ya ujangili imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa
ikilinganishwa na ndovu 219 waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473 mwaka
2012. Aidha, majangili 1,354 wamekamatwa na pembe za ndovu 542 na silaha
mbalimbali 184 nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya Idara ya
Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala yaani Tanzania
Wildlife Agency (TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi wanyama pori na
mapambano dhidi ya ujangili.
Natoa pongezi nyingi kwa askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi na vyombo
vingine vya Serikali na raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na
mafanikio yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana na ujangili na
biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori zitaendelezwa kwa
nguvu zaidi mwaka ujao 2015 na miaka inayofuatia. Napenda kutumia fursa hii
kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu wa maendeleo wanaotuunga mkono kwa
hali na mali katika mapambano haya. Naomba waendelee kutusaidia.
Hali ya Uchumi Jumla
Ndugu wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri kwa uchumi wa taifa. Uzalishaji katika sekta nyingi
ulikuwa ni mzuri. Ndiyo maana tunategemea kuwa tutafikia au hata kuvuka
lengo tulilojiwekea la pato la taifa kukua kwa asilimia 7.4 mwaka huu. Mwaka
2013 pato la taifa lilikua kwa asilimia 7.3. Mfumuko wa bei uliendelea kushuka
na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014 ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwa
asilimia 6.0. Hali nzuri ya upatikanaji wa chakula nchini imesaidia sana kufanya
mfumuko wa bei kuendelea kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa
bei utaendelea kushuka na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.
Mauzo Nje
Ndugu Wananchi;
Mauzo nje yameendelea kuongezeka. Katika kipindi kilichoishia Oktoba 31, 2014,
Tanzania iliuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani
milioni 8,503.9 ukilinganisha na mauzo ya dola milioni 8,332.5 katika kipindi
kama hicho mwaka 2013. Mapato yetu yangekuwa makubwa zaidi kama bei za
kahawa, chai, korosho na pamba zisingeanguka au bei ya dhahabu nayo
isingepada.
Akiba ya Fedha za Kigeni
Ndugu Wananchi;
Akiba yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekani milioni 4,251.8 kwa
kipindi kilichoishia Novemba 30, 2014. Kiasi hicho kinatuwezesha kuagiza
bidhaa toka nje kwa miezi 4.1. Hii ni chini ya lengo letu la kuwa na akiba ya
fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa kwa miezi minne na nusu. Hata hivyo, sina
wasiwasi kabisa kwamba tofauti hii ndogo tutaweza kuiziba mwaka 2015.
Mapato ya Serikali
Ndugu Wananchi;
Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba, 2014
yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama hicho mwaka 2013 hadi
shilingi bilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo yalikuwa
asilimia 90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 4,459.7. Kwa
mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu mbalimbali zilizosababisha lengo
lisifikiwe katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2014/2015. Hatua
zipasazo zinaendelea kuchukuliwa kurekebisha mambo hayo ili katika nusu ya
pili ya mwaka huu wa fedha makusanyo yafikie lengo na ikiwezekana yazidi ili
kufidia pengo la nusu ya kwanza.
Takwimu Mpya za Pato la Taifa
Ndugu wananchi,
Ni utaratibu wa kawaida wa nchi zote duniani kuwa na mwaka unaotumika
kuwa kizio (base year) cha kukokotoa takwimu za Pato la Taifa. Ni utaratibu
wa kawaida pia kwa kila baada ya muda fulani mwaka wa kizio hubadilishwa.
Lengo ni kuboresha takwimu husika. Katika marekebisho hayo pia huingizwa
thamani ya bidhaa na huduma mpya katika pato la taifa na kuziondoa
zilizotoweka ili kutoa picha halisi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Katika miaka ya hivi karibuni nchi za Ghana (mwaka 2010), Nigeria (mwaka
2013) na Kenya (mwaka 2014) wamefanya marekebisho ya takwimu zao za
pato la taifa. Na sisi Tanzania tumefanya hivyo mwaka huu (2014). Hii ni mara
ya tano kwa nchi yetu kurekebisha takwimu za pato la taifa. Mara nne zilizopita
ilikuwa mwaka 1966, 1976, 1992 na 2001.
Ndugu wananchi;
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekamilisha marekebisho ya takwimu za pato la
taifa na kukokotoa takwimu mpya kwa kutumia mwaka 2007 kama mwaka wa
kizio. Kutokana na marekebisho yaliyofanyika, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni
shilingi trilioni 70 kwa kutumia bei za mwaka 2007. Ukitumia bei za mwaka
2001, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 53.17. Kuongezeka kwa
pato la taifa kumeongeza pia pato la wastani la kila Mtanzania kutoka shilingi
1,186,200 (sawa na US$ 742) kwa bei za mwaka 2001 hadi shilingi 1,560,050
(sawa na US$ 977) kwa bei za mwaka 2007.
Kilimo na Chakula
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Uzalishaji ulikuwa tani milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni
14.38 mwaka wa jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni 1.64. Kwa mujibu
wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani milioni 3.25. Katika ziada
hiyo, mahindi yanachangia tani milioni 1.55, mchele tani 794,000 na kiasi
kinachobakia kinachangiwa na mazao mengine ya chakula.
Ndugu wananchi;
Kuna jambo moja muhimu kuhusu ununuzi wa nafaka ambalo ningependa
kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga wote na mtama wote
unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua sehemu ndogo tu ya nafaka
ya ziada iliyozalishwa na hununua kwa ajili ya kuweka akiba ya taifa ya
chakula cha kutumika wakati wa dharura ya watu kupata tatizo la njaa. Aidha,
Wakala hununua kiasi kinacholingana na uwezo wa maghala yake kuhifadhi.
Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni kuhifadhi tani 246,000 ingawaje
tunaendelea kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa kuhifadhi tani
400,000 ifikapo 2015. Hivyo basi kwa Wakala kununua tani 292,415.41 mwaka
huu ina maana kwamba kiasi cha karibu tani 50,000 zinahifadhiwa nje ya
maghala kwa kutumia maturubai. Huu siyo utaratibu mzuri na haifai kuendelea
nao kwani kuna hatari ya nafaka hiyo kuharibika na kuzua mgogoro mkubwa
siku moja.
Ndugu wananchi;
Baada ya NFRA kununua tani 292,415.41 kuna takribani tani milioni 2.96 za
nafaka ya ziada ambayo iliyobaki mikononi mwa wakulima. Mategemeo yetu ni
kuwa wafanyabiashara wetu watanunua nafaka hiyo kwa ajili ya kuuza mijini na
kwingineko inakohitajika. Bahati mbaya mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka wa
jana, wafanyabiashara wetu hawakuweza kununua nafaka yote ya ziada ambayo
Serikali haikuweza kununua kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula.
Hali hii imezua tatizo ambalo Serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara
nchini hatuna budi kulitafutia majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko
mengine ndani na hata nje ya nchi ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa
ziada. Nimeagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda
na Biashara kukaa chini na kushirikiana na wafanyabiashara kulitafutia
ufumbuzi suala hili lenye maslahi makubwa kwa wakulima na nchi yetu kwa
jumla.
Ndugu Wananchi;
Katika mazingira haya, ninapopata taarifa ya kuwepo watu wanaotaka kuuza
mahindi nje ya nchi lakini wanawekewa vikwazo na maafisa wa Serikali
inanishangaza na kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya hivyo waache
mara moja na badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao kufanikisha azma
yao. Hali kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao wajitokeze kufanya
biashara hiyo. Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni kwamba pawepo na
utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi.
Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo.
Miradi ya Kimkakati
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2014 utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa mujibu wa
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 2015/16) umeendelea vizuri.
Tunayo matumaini makubwa kwamba katika mwaka 2015 miradi mingi
itakamilika.
Tuanze na Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo
hadi Dar es Salaam. Mradi huu unategemewa kukamilika Januari, 2015.
Utakapokamilika utatuwezesha kutimiza lengo letu la kuzalisha MW 2,780 za
umeme ifikapo 2016. Mipango ya kupata ardhi ya ujenzi wa mitambo ya
kuchakata gesi asili kuwa ya kumiminika (LNG) ili iweze kusafirishwa kwenda
kwenye masoko, inakwenda vizuri.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa kusambaza umeme vijijini
umeendelea vizuri na tumepata mafanikio makubwa yasiyokuwa na mfano wake
katika historia ya nchi yetu. Hadi kufikia Novemba, 2014, jumla ya vijiji 3,836
vimepatiwa umeme na vingine 1,500 vinategemewa kupatiwa umeme ifikapo
Juni, 2015. Hivyo basi, vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423 vya Tanzania Bara
vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa na asilimia 43 ya vijiji vyote nchini
vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi sasa wananchi milioni 17.3 nchi nzima
sawa asilimia 36 wamefikiwa na huduma ya umeme ikilinganishwa na watu
milioni 8.1 sawa na asilimia 18.4 waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo
mwaka 2012. Mwaka 2015 tunatarajia watu milioni 18.2 sawa na asilimia 38
watafikiwa na umeme. Kwa upande wa vijijini mwaka 2012 watu milioni 2.3
sawa na asilimia 7 walikuwa na umeme. Ifikapo Juni 2015, idadi hiyo
itaongezeka na kuwa milioni 7.4 sawa na asilimia 21. Haya ni mafanikio
makubwa kwa wananchi wengi vijijini na mijini kupata umeme katika kipindi
kifupi kiasi hiki. Ni mageuzi ya aina yake yatokayotoa mchango muhimu katika
kuinua hali za maisha ya Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Tunaanza kuiona nuru ya matumaini kwamba siku si nyingi kutoka sasa, makaa
ya mawe ya Mchuchuma na madini ya chuma ya Liganga yataweza kutumika
kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wa Ludewa. Maandalizi yote muhimu
yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015 kuanza ujenzi wa mgodi wa makaa ya
mawe kule Mchuchuma, mtambo wa kufua umeme, ujenzi wa mgodi wa chuma
kisichoyeyushwa pale Liganga na ujenzi wa kiwanda cha kuyeyusha chuma.
Natoa pongezi maalum kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wabia
wenzao, Kampuni ya Sichuan Hongda ya China kwa hatua iliyofikiwa.
Inakadiriwa kuwa miradi hii ikikamilika itatoa ajira 33,000 za moja kwa moja na
zisizokuwa za moja kwa moja.
Ndugu Wananchi;
Mradi mwingine mkubwa wa kimkakati ni ule wa kujenga Eneo Maalumu la
Kiuchumi (Special Economic Zone) la Mbegani, Bagamoyo. Kwa mujibu wa
mpango kazi wa wabia wa mradi huo yaani Mamlaka ya Kuendeleza Maeneo
huru ya Uwekezaji (EPZA), Kampuni ya China Merchants Holdings International
na Mfuko wa Uhifadhi wa Akiba ya Mali za Serikali ya Oman (Oman State
General Reserve Fund), ujenzi wa bandari na miundombinu mingine
itakayowezesha viwanda kujengwa imepangwa kuanza Julai 2015.
Miundombinu ya Usafiri na Uchukuzi
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga barabara za lami na kuimarisha
barabara za udongo ili ziweze kupitika wakati wote ziliendelea kote nchini. Huu
nao ni mradi mkubwa wa kimkakati. Barabara za lami 19 zenye urefu wa
kilometa 1,459 zimekamilika kujengwa mwaka huu katika Mikoa ya Ruvuma,
Mbeya, Rukwa, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, Morogoro, Arusha,
Tabora na Shinyanga. Ujenzi unaendelea kwa barabara nyingine 24 katika
mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa, Simiyu, Katavi, Tabora,
Mwanza, Dar es Salaam, Kagera na Pwani ambazo wakati wo wote mwaka
2015 zitakamilika. Maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara nyingine nane
yanaendelea vizuri sehemu mbalimbali nchini.
Kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara, tumeendelea kufanya kazi ya ujenzi
na ukarabati wa barabara za udongo kote nchini. Mwaka huu Mfuko huo
umetengewa shilingi bilioni 751.7 ukilinganisha na shilingi bilioni 504.4 mwaka
jana. Aidha, mwaka huu tumeweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto
Kilombero. Matumini yetu ni kuwa ujenzi wa daraja hilo na Daraja la Kigamboni
utakamilika mwaka 2015. Ujenzi wa Daraja la Malagarasi ulishakamilika mwaka
jana, kinachosubiriwa ni sherehe ya uzinduzi.
Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, tunategemea kukamilisha ujenzi wa
Awamu ya Kwanza ya barabara za mabasi yaendayo kasi. Ni matarajio yetu pia
kwamba mabasi yataanza kusafirisha abiria katika kipindi cha nusu ya kwanza
ya mwaka 2015. Halikadhalika, tunategemea katika mwaka 2015 ujenzi utaanza
wa barabara zinazozunguka jiji la Dar es Salaam (ring roads), barabara ya
Mwenge - Morocco na ile ipitayo juu ya nyingine (flyovers) eneo la TAZARA.
Vile vile, daraja jipya la Salenda litaanza kujengwa. Aidha, kivuko cha abiria 300
cha MV Dar es Salaam kitaanza kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam
Kaskazini na Ferry mapema mwakani. Hatua zote hizi zinalenga kupunguza
msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Usafiri wa Anga na Reli
Ndugu wananchi;
Jitihada za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati zimeendelea kwa
mafanikio. Mwaka huu vichwa vinane vya treni vimekarabatiwa, mabehewa
mapya 22 ya abiria na mabehewa 274 ya mzigo yamenunuliwa. Mabehewa hayo
yameanza kuwasili nchini kati ya Novemba na Desemba mwaka huu. Kati ya
Januari na Mei, 2015 tunatarajia kupokea vichwa vipya vya treni 13. Uboreshaji
huu wa huduma za treni unakwenda sambamba na ukarabati wa reli yenyewe,
ujenzi wa madaraja na kuimarisha maeneo yaliyo korofi katika reli hiyo.
Kuhusu ujenzi wa reli iliyo pana zaidi (standard guage), yenye uwezo wa
kubeba mabehewa mengi na kuwezesha treni kwenda kwa mwendo wa kasi
zaidi, juhudi za kutafuta fedha za ujenzi au wabia wa kushirikiana nasi kujenga
zinaendelea. Wakati huo huo, tunaendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa
matatizo ya reli ya TAZARA ili mambo yaende vizuri. Tutashirikiana kwa karibu
na wabia wenzetu wa Zambia. Bahati nzuri Serikali ya China iko tayari kuunga
mkono juhudi zetu za kufufua reli ya TAZARA.
Usafiri wa Anga
Ndugu Wananchi;
Sekta ya usafiri wa anga imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi ya abiria
wanaowasili na kutoka katika viwanja vyetu vya ndege nchini imeongezeka
kutoka abiria milioni 2.5 mwaka 2013 hadi abiria milioni 3.5 kufikia Septemba,
2014. Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi za nje zimeongezeka kutoka
274 Januari, 2013 hadi 295 kufikia Septemba, 2014. Hili ni ongezeko la asilimia
8. Safari za ndege ndani ya nchi nazo zimeongezeka kutoka safari 230,458
mwaka 2013 hadi safari 241,922 mwaka 2014. Hii ni sawa na ongezeko la
asilimia 39. Maongezeko haya ni kielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii
na biashara nchini zimeendelea kukua.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa Jengo la 3 (Terminal 3) la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea vizuri. Jengo hilo litakapokamilika
mwakani, litakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa abiria milioni 8 kwa
mwaka. Aidha, ukarabati wa Jengo la 2 (Terminal 2) utafanyika ili liweze kutoa
huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na ujenzi huo, Wakala wa Viwanja vya
Ndege wameendelea kukarabati na kuboresha viwanja vya ndege vya KIA,
Mwanza, Songwe, Bukoba, Tabora na Kigoma. Tunatarajia ukarabati wa viwanja
vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga kuanza mapema mwaka 2015.
Elimu
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupiga hatua za kuridhisha katika kuboresha elimu nchini.
Tumefanikiwa kupunguza tatizo la upungufu wa maabara, vitabu na walimu wa
shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeajiri walimu 36,339 kati ya
81,562 wanaohitajika. Tumebakiwa na upungufu wa walimu 45,223 yaani 26,946
wa shule za msingi na 18,277 wa shule za sekondari hususan wa masomo ya
sayansi. Hivi sasa hatuna tatizo la walimu wa masomo ya sanaa katika shule
za sekondari.
Mwaka huu tumeanza mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya Diploma ya
Ualimu kwa masomo ya sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma
ambapo jumla ya wanafunzi 5,602 wa masomo hayo wamedahiliwa. Mpango
huu utatuwezesha kupunguza pengo kubwa tulilonalo la walimu wa sayansi
katika muda mfupi zaidi.
Ujenzi wa Maabara
Ndugu wananchi;
Ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari za
Kata 3,463 umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa zijengwe
maabara 10,389 ilipofika Novemba, 2014. Taarifa kutoka TAMISEMI
zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 29, 2014, maabara 4,207 sawa na
asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688 sawa na asilimia 54.8
zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na maabara 494 sawa na
asilimia 4. zilikuwa katika hatua za awali za ujenzi.
Ndugu Wananchi;
Natoa pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti na
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini pamoja na
wananchi, kwa jitihada kubwa iliyofanyika. Kwa kutambua jitihada hizo,
nimeongeza miezi sita zaidi kwa wale ambao hawajakamilisha ujenzi wa
maabara hizo wafanye hivyo. Sikusudii kuongeza tena muda baada ya hapo.
Naomba watumie kipindi hicho kitumike kutafuta vifaa vya maabara. Serikali
itasaidia upatikanaji wa watunza maabara (laboratory technicians) ambao
tumeanza programu kubwa ya mafunzo yao na mahitaji mengine ya maabara.
Ununuzi wa Vitabu
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya kufundishia
katika shule za msingi na sekondari. Tumekuwa tunanunua vitabu kwa kutumia
Bajeti ya Serikali na misaada kutoka kwa marafiki zetu wa maendeleo. Kwa
mfano, Serikali ya Marekani imetupatia vitabu milioni 2.5 vya masomo ya
sayansi na hisabati kwa shule za sekondari. Ongezeko hili la vitabu linashusha
uwiano uliopo sasa wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne na kufikia kitabu
kimoja kwa wanafunzi wawili. Lengo letu ni kila mtoto kuwa na kitabu chake
kwa kila somo ifikapo mwaka 2016.
Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Ndugu wananchi;
Mafanikio mengine tuliyopata mwaka huu ni kukamilika kwa Sera ya Elimu na
Mafunzo ya mwaka 2014. Hii ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya elimu
nchini hakuna badala yake. Sera mpya inalenga kuinua ubora wa elimu na
mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha Watanzania wengi
zaidi kupata fursa za elimu iliyo bora na inayolinga na wakati tulionao. Jambo
jipya sana na la kihistoria katika Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya
kuondoa ada katika elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa
hatuna ada kwenye shule za msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa
elimu ya sekondari. Kwa mujibu wa maelezo hayo ya Sera, nimekwishatoa
maagizo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango kuanza
kutafakari namna jambo hilo litakavyotekelezwa.
Afya
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2014 jitihada za kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania
ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na mlipuko wa homa ya dengue
iliyowapata watu 1,039 na kusababisha vifo vya watu 3 kati yao. Kwa upande
wa maradhi ya ebola tumejiandaa vya kutosha kutambua watu wenye maradhi
hayo wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege vya kimataifa na vituo vyote
vya mpakani. Aidha, tumejipanga vyema kuwahudumia wagonjwa wa maradhi
hayo iwapo watatokea.
Mwaka huu pia, Madaktari wetu watano wamekwenda Liberia kusaidiana na
ndugu zetu wa huko katika kukabiliana na ugonjwa wa ebola. Madaktari wetu
hao wako salama na wanaendelea vizuri kutoa huduma. Madaktari hao
watakaporejea nchini watakuwa hazina kubwa ya taifa katika kupanga mipango
ya kukabiliana na ugonjwa huu hatari. Hali kadhalika, watakuwa viongozi wa
wengine katika kutibu wagonjwa wa maradhi ya ebola iwapo watatokea nchini.
Ndugu Wananchi;
Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri watumishi wa
sekta ya afya 8,345 ambao kati yao kuna madaktari 244, madaktari bingwa 75,
wauguzi 2,555 na wataalamu wa kada nyingine za afya 5,471. Mwaka huu pia
tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 7,956 katika
mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi 9,730. Kwa ongezeko hilo, sasa tumefikia
asilimia 97 ya lengo letu la kudahili wanafunzi 10,000 ifikapo mwaka 2017.
Jitihada zetu za kuongeza fursa za mafunzo kwa Madaktari, Wauguzi na
wataalamu wengine wa afya zina muelekeo mzuri. Ujenzi wa hospitali ya
kufundishia pale Mloganzila unaendelea vizuri na hospitali ya kufundishia ya
Chuo Kikuu cha Dodoma umekamilika. Ni matarajio yangu kuwa wakati wo wote
mwakani ujenzi wa kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila
utaanza. Ujenzi huo ukikamilika Chuo kikuu cha Muhimbili kitaweza kudahili
wanafunzi 12,000 kutoka wanafunzi 2,500 wa sasa jambo ambalo litafanya
upungufu wa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wa Afya kupata jawabu la
uhakika. Tumeendelea kufanya mambo mengine ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba
za ubongo na mishipa ambalo limekamilika pale Muhimbili, sasa tunahangaikia
kupata vifaa.
Maji
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu wa 2014 tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya
kuwapatia wananchi maji safi na salama mijini na vijijini. Kwa ajili hiyo miradi
498 ya maji vijijini imekamilika na miradi 740 ipo katika hatua mbalimbali za
ujenzi. Miradi mingine 378 ipo katika maandalizi ya ujenzi kuanza. Ni matarajio
yetu kwamba katika mwaka ujao wa 2015, miradi mingine 731 itatekelezwa na
vituo 25,790 vya kuchota maji vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza
kuwafikia asilimia 71 ya wananchi wanaopata maji safi na salama vijijini kutoka
asilimia 58 ya sasa. Kwa ajili hiyo, tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la
kuwapatia watu maji asilimia 65 ya Watanzania waishio vijijini ifikapo 2015.
Ombi langu kwa ndugu zetu wa Hazina waiangalie sekta hii ya maji kwa
ukaribu zaidi na wawapatie fedha kwa wakati.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga Same Mkomazi pamoja
na miji na vijiji vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015. Fedha
zimekwishapatikana na Mkandarasi wa Awamu ya Kwanza ameshapatikana.
Makandarasi wa Awamu ya Pili na Tatu watapatikana muda si mrefu kutoka
sasa. Hii pia itahusu kupata Mkandarasi wa mradi wa maji wa mji wa
Orkesment.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu miradi ya kuipatia maji miji kadhaa nchini ilikamilika na tatizo la
upungufu wa maji litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ipo miji kadhaa ambayo miradi
imefikia hatua ya juu na kwamba wakati wowote mwakani itakamilika. Jiji la
Dar es Salaam lipo katika kundi hili. Kazi ya upanuzi wa miradi ya maji ya Ruvu
Juu na Ruvu Chini kwa msaada wa Serikali ya Marekani na mkopo kutoka
Serikali ya India imefikia hatua nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika nusu ya
kwanza ya mwaka 2015. Mwaka ujao pia visima virefu vya Kimbiji na Kipera
vitachimbwa na Bwawa la Kidunda litaanza kujengwa.
Serikali ya India pia imekubali kutupatia mkopo wa Dola za Marekani milioni
268.2 kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji miji ya Tabora, Nzega na
Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa kujumuisha miji ya Sikonge na
Urambo katika mradi huo utaangaliwa.
Bunge na Mahakama
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2014, mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea kutekeleza
vyema majukumu yao. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza
kuendesha shughuli zake kama ilivyopangwa pamoja na kulazimika kugawana
Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum la Katiba. Bunge limefanya mikutano
mitatu, Miswada 17 ya Sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza, Sheria tano na
maazimio saba yalipitishwa. Maswali ya msingi 569 na ya nyongeza
1,541yaliulizwa na kujibiwa. Aidha, sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow nalo
lilijadiliwa na kutolewa maazimio. Tumeshaanza kuchukua hatua kuhusu
maazimio hayo na bado tunaendelea.
Napenda kuitumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wabunge wetu kwa
kutekeleza vizuri wajibu wao wa Kutunga Sheria na kusimamia Serikali.
Nawasihi waendelee na msimamo huo mwema na chanya kwa maslahi ya nchi
yetu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mahakama napenda kutambua kazi kubwa na nzuri
inayofanywa ya kupunguza mrundikano wa mashauri katika Mahakama za ngazi
zote. Wahenga wamesema mcheza kwao hutunzwa. Hatuna budi kutoa pongezi
maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kwa uongozi
wake mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa
Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo
wamejiwekea malengo ya kusikiliza na kutoa hukumu kwa mashauri
yasiyopungua 200 kwa mwaka kila mmoja wao.
Habari njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea vizuri.
Mashauri 870 yalisikilizwa na kuamuliwa kwenye Mahakama ya Rufani,
mashauri 11,334 kwenye Mahakama Kuu, mashauri 8,715 kwenye Mahakama ya
Mahakimu Wakazi na Mashauri 25,683 katika Mahakama za Wilaya. Aidha,
mkakati wa kupeleka timu ya Majaji wa Mahakama Kuu kwa wakati mmoja
kwenye maeneo yenye mashauri mengi kama ilivyofanyika Kigoma, Shinyanga
na Tabora umesaidia sana kupunguza mrundikano wa mashauri ya siku nyingi.
Haijawahi kutokea mashauri mengi kiasi hicho kusikilizwa na kumalizwa katika
historia ya Mahakama nchini.
Ndugu Wananchi;
Mkakati huu mpya umeleta matumaini mapya kwamba tatizo la kuchelewesha
kwa mashauri ambalo lilidhaniwa kuwa ni tatizo sugu sasa limeanza kupatiwa
ufumbuzi. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote natoa shukrani na pongezi
nyingi kwa Jaji Mkuu, Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu
na Mahakimu wa ngazi zote kwa kazi nzuri waifanyayo.
Hali kadhalika, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama na watendaji wote
wa Mahakama kwa kazi nzuri waifanyayo ya kuwawezesha Majaji na Mahakimu
kutimiza ipasavyo majukumu yao. Hakika utendaji Mahakamani umebadilika na
kuwa bora zaidi. Mimi naahidi kuendelea kusaidia Mahakama kwa kuwahimiza
ndugu zetu wa Hazina kutoa kwa wakati pesa zilizotengwa katika bajeti.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yameendelea
bila ya ajizi. Katika mwaka huu wa 2014 TAKUKURU wamepokea taarifa 237 na
wamekamilisha uchunguzi wa mashauri 545. Watuhumiwa waliofikishwa
Mahakamani ni 428. Mashauri yaliyomalizika ni 205, kati ya hayo 125
watuhumiwa waliachiliwa na 80 walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Mwaka
huu wa 2014 mali na fedha taslimu zenye thamani ya shilingi bilioni 38.96
zimeokolewa. Katika kuimarisha Taasisi hiyo kiutendaji, maafisa wapya 394
wameajiriwa.
Sherehe za Miaka 50 ya Muungano
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu wa 2014 tuliadhimisha miaka 50 ya Muungano wa nchi zetu mbili
yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kwa heshima
inayostahili. Maadhimisho yalifikia kilele tarehe 26 Aprili, 2014 na zilifanyika
sherehe nchini kote na sherehe hizo zilifana sana. Ni ukweli usiopingika kuwa
kwa Muungano wetu kuweza kudumu kwa nusu karne ukiwa bado imara na
unazidi kustawi ni mafanikio makubwa. Matumaini kwa siku za usoni ni mazuri.
Naamini Muungano wetu utaimarika zaidi iwapo Katiba Inayopendekezwa
itapitishwa kwani yale mambo yenye kuleta matatizo hivi sasa yatakuwa
yamepatiwa ufumbuzi.
Miaka 50 ya JWTZ
Ndugu Wananchi;
Wakati nchi inasherehekea miaka 50 ya Muungano, baadhi ya vyombo na
taasisi muhimu kitaifa zilifanya hivyo hivyo. Miongoni mwa walioadhimisha
nusu karne ya kuundwa kwake ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kama
mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe 1 Septemba, 1964. Jeshi letu liliadhimisha siku
yao hiyo kwa kufanya zoezi kubwa la kivita lililoanza Kibaha mkoani Pwani na
kumalizikia Monduli Mkoani Arusha.
Nilibahatika kushuhudia siku ya mwisho ya zoezi hilo. Nilifurahishwa sana na
kiwango cha utayari kivita cha Jeshi letu. Wanajeshi wetu walionesha weledi wa
hali ya juu, umahiri mkubwa, ujasiri, ukakamavu na uvumilivu wa aina yake
wakati wa kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu ya uwanja wa
medani za vita. Niliwapongeza siku ile na narudia tena leo kuwapongeza.
Niliyoyaona yamenihakikishia mimi na Watanzania wote kuwa Jeshi letu la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liko imara kulinda mipaka ya nchi yetu na
kuhakikisha usalama wa taifa letu na watu wake. Jeshi letu bado ni lile
tunalolijua sisi sote, lakini limezidi lile lililomngoa mvamizi Dikteta Iddi Amin wa
Uganda, tena limezidi kwa mbali.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu pia tumeshuhudia kukamilika kwa zoezi muhimu la kuandika Katiba
Inayopendekezwa. Kama tujuavyo sote, mchakato uliozaa Katiba
Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi ndani na nje ya Bunge Maalum
la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo lilikamilisha kazi yake kwa salama siku
mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba, 2014 ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho.
Mimi na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein tulikabidhiwa
nakala za Katiba Inayopendekezwa tarehe 8 Oktoba, 2014. Nimeshatimiza
wajibu wangu wa kuchapisha katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya
kupiga kura ya maoni kuwa tarehe 30 Aprili, 2015. Nimeshatoa maagizo kwa
Tume ya Uchaguzi kufanya matayarisho husika ya kuwezesha Kura ya Maoni
kufanyika.
Ndugu Wananchi;
Moja ya mambo muhimu ambayo Tume ya Uchaguzi inafanya kwa sasa ni
kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Mpiga Kura. Tume imeamua kutumia
mfumo mpya wa Biometric Voters Register. Uandikishaji wa majaribio
umefanyika katika baadhi ya Kata katika Majimbo ya Mlele, Kawe na Kilombero.
Matatizo yaliyojitokeza yatasaidia kuboresha mfumo huo kabla ya uandikishaji
wa watu wote wenye sifa stahiki kuanza.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuwafahamisha Watanzania wenzangu wote kuwa
mfumo mpya unatengeneza Daftari Jipya la Mpiga Kura ingawaje lugha
inayotumika ni uboreshaji wa Daftari la sasa. Uboreshaji huu wa Daftari la
Mpiga Kura ni tofauti na ule tuliouzoea ambapo walikuwa wanaandikishwa
wapiga kura wapya na wale waliopoteza vitambulisho vyao. Safari hii
wanaandikishwa wote wapya na wa zamani na wote watapata vitambulisho
vipya. Hivyo basi, sisi wenye vitambulisho vya kupiga kura vya zamani
tusifanye ajizi, tujitokeze kujiandikisha wakati ukifika.
Jambo la pili ni kwamba, Daftari la Mpiga Kura linalotayarishwa siyo kwa ajili
ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa peke yake, daftari hilo hilo
litatumika pia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo basi,
kujiandikisha ni jambo muhimu sana. Usipofanya hivyo siyo tu utajinyima fursa
ya kushiriki kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa bali pia utakosa fursa ya
kuchagua Rais wako, Mbunge wako na Diwani wako. Katu usikubali yakukose
hayo.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo tarehe 14 Desemba, 2014 na 20 Desemba, 2014 ulifanyika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa.
Uchaguzi umekwisha na viongozi wamekwishapatikana. Sasa ni wajibu wa
viongozi hao kufanya kazi waliyoiomba. Kwa walioendesha uchaguzi ni wakati
mzuri wa kufanya tathmini ili wapate mafunzo yatokanayo na uchaguzi huo.
Kwa TAMISEMI na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, lengo liwe ni kuona
namna ya kuimarisha mazuri na kusahihisha makosa na matatizo
yaliyojitokeza. Kwa walinzi wa amani watambue matatizo ya kiusalama
yaliyotokea na kuona namna ya kutengeneza mikakati ya kuzuia matatizo ya
namna hiyo yasijitokeze tena. Hatma ya yote, shabaha yetu ni kutaka kufanya
vizuri zaidi katika chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa na kufanya vizuri zaidi
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Ni zamu yetu kwa mujibu wa mzunguko wa uongozi wa Jumuiya
yetu kati ya nchi wanachama. Ni dhamana kubwa na kwamba wenzetu wa
Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze katika kutekeleza malengo na
madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa katika Mkataba ulioanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika, tunategemewa kuongoza katika
utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya vikao vya Jumuiya. Hii inahusu
maamuzi yaliyokwishafanywa kabla yetu ambayo utekelezaji wake unaendelea
na uamuzi mpya utakaofanywa katika kipindi cha uongozi wetu.
Kwa niaba ya Watanzania wote napenda kuwashukuru ndugu zetu wa Burundi,
Kenya, Rwanda na Uganda kwa kutuamini. Napenda kuahidi kuwa
hatutawaangusha. Sisi Watanzania tutafanya kila tuwezalo kuimarisha Jumuiya
ya Afrika Mashariki kwa manufaa ya Jumuiya yenyewe, nchi zetu na wananchi
wa Afrika Mashariki. Tutajitahidi kuwa wabunifu kwa nia ya kuona utangamano
unakua na kustawi kwa kasi na kuzaa matunda ya maendeleo tunayoyatarajia
sote. Matunda tuliyoyatarajia tulipoamua kuanzisha Jumuiya hii na matunda
tuliyoyapata tulipoamua kwa hiari yetu kujiunga nayo kuwa wanachama.
SADC, AU NA UN
Ndugu Wananchi;
Kuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika
na Umoja wa Mataifa, tunaahidi kuendelea kuwa wanachama waaminifu na
kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mashirika
haya ya kikanda na kimataifa. Kwa upande wa SADC tutaendelea kushiriki
katika utekelezaji wa mikakati na mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii
na ile ya kisiasa na kiusalama kama ilivyoainishwa katika RISDP (Regional
Indicative Strategic Development Plan) na SIPO (SADC Strategic Indicative Plan
for the Organ). Kwa ajili hiyo Tanzania, itaendelea kutoa mchango wake katika
kukuza utangamano wa kiuchumi katika SADC na kusaidia kuimarisha uhusiano
mwema na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa SADC. Hii ni pamoja
na kusaidia katika kutatua migogoro ya kisiasa na kusalama kati ya nchi
wanachama.
Kwa upande wa Umoja wa Afrika tutaendelea kutekeleza maamuzi ya vikao na
taasisi mbalimbali za Umoja huo. Daima tutakuwa wanachama waaminifu wa
Umoja wa Afrika na kuchangia katika uimarishaji wake. Kuhusu Umoja wa
Mataifa tutaendelea kutimiza wajibu wetu kama wanachama wa Umoja huo wa
kimataifa ulio adhimu na muhimu kwetu na dunia nzima. Tutaendelea kushiriki
katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunao
wanajeshi wetu katika majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika
nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan na Lebanon. Tuko tayari
wakati wote kuchangia zaidi iwapo Umoja wa Mataifa watatutaka tufanye
hivyo.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Namaliza hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa
kuiunga mkono Serikali yetu na kwa mchango wenu uliowezesha nchi yetu
kupata mafanikio haya makubwa tunayojivunia katika mwaka 2014. Tumeweza
kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu mengi. Umoja wetu na mshikamano
wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza mwaka 2015 kwa
matumaini makubwa. Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya kuendelea
kuliimarisha zaidi taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo
huenda ukawa na changamoto na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka huu.
Uelewa wetu, umoja wetu, mshikamano wetu na moyo wetu wa uzalendo ndivyo
vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. Mimi nina imani
kubwa kwa uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa nzuri
ya nchi yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na utulivu.
Tumeweza mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na miaka
ijayo. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka mpya.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza.
Post a Comment